Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 13:56

Mahakama Kenya yawakuta na hatia maafisa wa ngazi ya juu


Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang'i .
Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang'i .

Mahakama ya Juu nchini Kenya imewakuta na hatia Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang'i, Inspekta Jenerali wa Polisi Joseph Boinnet na Katibu Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Gordon Kihalangwa kwa kosa la kutofuata maagizo ya mahakama.

Hili linafuatia uamuzi wa serikali ya Kenya kwa siku ya tatu mfululizo kuendelea kumshikilia wakili wa Upinzani Miguna Miguna anayeendelea kuzuiliwa katika Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi hata baada ya mahakama Jumanne kuagiza aachiliwe huru.

Jaji wa mahakama hiyo George Odunga amewaamrisha viongozi hao watatu kufika mbele ya mahamaka kupokea hukumu Alhamisi asubuhi.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili anaripoti kuwa kwa siku ya tatu mfululizo Miguna Miguna anaendelea kuzuiliwa katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta tangu alipoingia Kenya kutoka Toronto Canada.

Kizuizi cha kuruhisiwa kuingia Nairobi kikiwa kushindwa kwake kusalimisha Pasipoti yake ya Canada ili kupokea stakabadhi za uraia wa Kenya ambao serikali ya Kenya inaeleza iliupoteza mwaka wa 1988.

Lakini darubini imerejea mahakamani ambako cheche za miale ya moto zimekuwa zikihanikiza. Serikali ya Kenya ikitakiwa na mahakama kumuachilia mara moja wakili huyo wa Upinzani. Agizo ambalo serikali imelikaidi.

Na kufuatia agizo la Jaji wa Mahakama Kuu Roselyn Aburili la kumtaka serikali kumfikisha Miguna mahakamani leo asubuhi kupuuzwa, Jaji George Odunga anawaonya maafisa wa ngazi ya juu serikalini dhidi ya mazoea ya kuendelea kukaidi amri zake.

Jaji Odunga amesema: "Maafisa hawa wanatakiwa kufika mbele ya mahakama hii kesho saa nne asubuhi,kupokezwa hukumu na kupata maagizo mengine.Na Iwapo watakosekana,mahakama hii itatangaza adhabu ya kiwango cha hukumu."

Jaji Odunga ameionya serikali dhidi jaribio la kupambana na nguvu za mahakama akieleza kuwa afisa yeyote serikalini anayekaidi maagizo ya mahakama atakabiliwa na msumeno wa sheria.

Ameongeza kuwa mbali na kubaini iwapo maamuzi yake yameafikiwa, mahakama hii ni sharti ihakikishe kuwa amri zake zinafuatwa.

"Kesi mbele yangu sasa ya watu husika imefika kiwango ambacho nguvu za mahakama zinajaribiwa na heshima ya mahakama inachunguzwa. Mahakama haitakunja mbawa yake huku washtakiwa wanatembea kwa madaha na kupuuza maagizo.

Aidha, Jaji Odunga anaitaka serikali ya Kenya kumuachilia Miguna Miguna mara moja.

"Mlalamikaji hataondolewa katika mikono ya mahakama kwa hali yoyote ile. Badala yake anafaa kuachiliwa huru bila masharti yoyote na kufika mbele ya mahakama hii kesho saa nne asubuhi," Jaji Odunga amesisitiza.

Miguna ambaye alijitangaza kuwa kiongozi wa VuguVugu la National Resistance Movement kabla ya kulazimishwa kwenda uhamishoni, alikamatwa na kuzuiliwa na polisi kwa takriban siku tano kwa kushiriki hafla ya kumlisha kiapo kiongozi wa upinzani, Raila Odinga.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennedy Wandera, Kenya

XS
SM
MD
LG