Mwili wa Ruge waagwa kitaifa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli ameungana Jumamosi na viongozi wengine kitaifa akiwemo Rais mstaafu Jakaya Kikwete kutoa heshima zao za mwisho kwa Marehemu Ruge Mutahaba.
Magufuli aliwaongoza maelfu ya waombolezaji kuuaga mwili wa marehemu kwenye hafla ya kumuenzi Ruge iliyofanyika katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam, Jumamosi March 2, 2019
Mkuu wa Mkoa aongoza mapokezi
Siku ya Ijumaa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda naye aliongoza mapokezi hayo ya huzuni ambayo ilikuwa wazi kuwa Ruge alikuwa amezikonga nyonyo za watu wengi wakati wa uhai wake.
Maelfu ya waombolezaji walijitokeza na kusubiri katika vituo vyote 11 vilivyopangwa mwili huo kupita hadi kwenye Hospitali ya Lugalo, jijini ulikohifadhiwa.
Kwa kufuata ratiba iliyokuwa imetolewa msafara huo ulipita katika vituo 11 vilivyokuwa vimetajwa katika ratiba ya maziko ambavyo ni Barabara ya Nyerere, Buguruni, Karume, Magomeni, Hoteli ya Morocco, Sinza Kijiweni, Bamaga, ITV, Clouds, Kawe na Hospitali ya Lugalo.
Wakati msafara huo unaingia eneo la Magomeni, ulilazimika kusimama kwa muda na Mkuu wa Mkoa (Makonda) alilazimika kutoa maelekezo kwa waendesha pikipiki waliokuwa wameizingira gari iliyobeba mwili wa Ruge kuacha kusababisha foleni na hivyo kuchelewesha msafara kwenda ilivyopangwa.
Msafara huo ulipofika Tandale idadi ya watu iliongezeka na kuwa na msongamano mkubwa wa magari hadi kwenye maeneo ya Sinza.
Pia, baadhi ya wananchi walijitokeza pembezoni mwa barabara hizo na mabango yenye ujumbe wa kumuenzi Ruge.
Kuwasili kwa mwili wa marehemu Clouds
Mara baada ya mwili wa Ruge kuwasili kwenye ofisi za Clouds zilizoko Mikocheni jijini Dar es Salaam, huzuni ilitanda na vilio vilisikika kwa nguvu kutokana na majonzi ya kufa kwa kiongozi wa kituo hicho mwenye kutolewa mfano na watu wa rika zote.
Mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vilionyesha mapokezi hayo mubashara mara baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa Dar es Salaam, mwili huo uliingizwa kwenye gari maalum la kubeba maiti lenye namba za usajili T 195 DGZ na msafara ulianza kwenda Hospitali ya Jeshi Lugalo saa 10:00 jioni, saa za Afrika Mashariki.
Ruge (48), alifariki dunia Jumanne Afrika Kusini ambako tangu mwishoni mwa mwaka 2018, alikuwa anapatiwa matibabu maalum kutokana na maradhi ya figo.
Ilipofika Saa 12.48 jioni, saa za Afrika Mashariki, mwili huo uliondolewa kwenye ofisi hizo na kupelekwa Hospitali ya Jeshi Lugalo.
Gwajima atoa salaam za rambirambi
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, aliwaambia waombelezaji waliyofika nyumbani kwa marehemu kuwa Ruge ameondoka kabla kipaji chake haijatumika kikamilifu.
Alisema : "Taa ya Clouds Media imezimika katikati ya giza, hivyo chombo hicho cha habari kinapaswa kujipanga namna ya kutoka gizani.