Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Februari 01, 2023 Local time: 18:22

Magufuli asema kuongezwa kipindi cha urais ni kukiuka Katiba


Rais wa Tanzania John Magufuli amesema anasikitishwa na hafurahishwi na mjadala ambao unaoendelea wa rais kuongezewa kipindi cha kutumikia kutoka miaka mitano hadi saba.

Amesema kuwa kufanya hivyo ni kinyume na Katiba ya nchi na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Rais alitoa kauli hiyo Ikulu, Dar es Salaam Jumamosi alipokutana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Humphrey Polepole.

Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, amewataka wananchi kupuuza mjadala huo.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Ikulu, Rais alimwagiza Polepole kuwajulisha wanachama wa CCM na Watanzania kuwa anasikitishwa na hafurahishwi na mjadala huo.

“Rais Magufuli amewataka wanachama wa CCM na umma wa Watanzania kwa ujumla kupuuza mjadala huo kwa kuwa haujawahi kujadiliwa katika kikao chochote cha chama na ni kinyume na Katiba ya CCM na Katiba ya nchi,” alisema Polepole.

Polepole alisema Magufuli aliwataka wana CCM na umma wa Watanzania kutokubali kuyumbishwa ama kupotoshwa na mambo yasiyokuwa ya msingi, badala yake wajielekeze katika ajenda muhimu ya kujenga uchumi na kutekeleza Ilani ya CCM iliyonadiwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Pia alisema Magufuli hana mpango wowote na hatarajii kuongeza kipindi cha urais wakati wote wa uongozi wake.

Kauli ya Magufuli inajibu hoja za baadhi ya viongozi, wakiwamo wabunge ambao mara kadhaa walikaririwa wakitaka kuongezwa kwa ukomo wa urais na ubunge hadi kufikia miaka saba ili kumpatia rais na wabunge muda wa kutekeleza majukumu yao.

Hoja ya kuongeza ukomo wa urais ilianza kuibuliwa Septemba 12, mwaka jana na Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM), alipowasilisha kusudio lake la muswada binafsi wa mabadiliko ya Katiba unaohusu kuongeza ukomo wa Bunge.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG