Riporti hiyo iliyowasilishwa kwa rais Samia Suluhu Hassan Jumatano, inaonyesha upotevu wa fedha za serikali ukiendelea.
Baadhi ya wachumi wanaitaka serikali kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale ambao wametajwa na kuhusishwa katika ripoti hiyo, na kuongezea kuwa ni vyema wasimamishwe kazi ili uchunguzi wa kina ufanyike.
Katika kipindi cha mwaka jana na mwaka huu kasoro zimeongezeka katika maeneo mbalimbali kwenye mamlaka za serikali.
Akitoa mfano wa shirika la ndege Tanzania ATCL, mchumi Walter Nguma aliaambia sauti ya Amerika kuwa ripoti hiyo imeonyesha ufisadi mkubwa uliofanyika katika shirika hilo ambalo limekuwa likijiendesha kwa hasara kutoka bilioni 22 mpaka bilioni 37.
“Madudu yameongezeka zaidi ukiangalia ATCL mwaka jana na mwaka huu unaona ripoti hii ndio imefanya madudu zaidi kutoka kwenye bilioni 22 hasara tumeenda mpaka bilioni 37 ni ripoti ambayo imezingatia uandishi lakini ni madudu kila mahali sio ripoti yakuweza kuonyesha nia thabiti,” amesema Nguma.
Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanasema dhana ya kupambana na ufisadi inaanzia utiifu wa maadili ya uongozi na kuweza kufahamu jinsi ya kudhibiti mianya ya rushwa inayotumiwa na baadhi ya watu wachache ambao ni wabadhirifu wa mali za umma.
Akizungumzia suala la viongozi wa serikali kutumia mali za umma kwa manufaa binafsi, Nassoro Kitunda mchambuzi wa masuala ya uchumi na pia ni mhadhiri msaidizi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam amesema ni muhimu maadili ya uongozi yapewe kipaumbele na sheria kali ziwepo ili kupambana na ubadhirifu.
“Ifike mahala tuseme wazi kwamba kama unataka kuwa kiongozi uwe kiongozi kama unataka uwe mfanya biashara basi baki na biashara zako”alisema Kitunda.
Hata hivyo Azizi Rashidi ambaye ni mtafiti wa masuala ya uchumi wa fedha na benki kutoka Dar es Salaam aliiambia sauti ya Amerika kuwa maeneo mengi ya mamlaka za serikali yanahitaji ufuatiliaji na kutilia mkazo suala la uwajibikaji kwa watumishi waliopewa madaraka ya kuongoza.
“Kama pana kitu kinatakiwa kiongezwe zaidi ni uwajibikaji wa watu walio pewa mamlaka ya kuzisimamia hizi taasisi au sekta kuwajibika” alisema Rashidi.
Mashirika ya umma ya kibiashara 14 yalipata hasara katika mwaka wa fedha 2021/2022, miongoni hayo ni shirika la ya Ndege la Tanzania ATCL iliyopata hasara ya Tsh. Bilioni 35.2 na Shirika la Reli TRC limepata hasara ya Tsh. Bil 31.2, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Kichere