Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Aprili 20, 2024 Local time: 09:57

Chadema kuendelea kushinikiza kuwepo demokrasia Tanzania


Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu amesema Tanzania ni nchi ya demokrasia na watu wake wakiwemo wanasiasa wanahaki ya kutoa mawazo yao na kukusanyika na kufanya mikutano ya hadhara.

Akizungumza kwenye makao makuu ya Chadema masaa machache baada ya kupewa dhamana Alhamisi Lissu amesema ilivyokuwa Tanzania ni nchi yenye misingi ya demokrasia, ataendelea kupigania kuwepo demokrasia nchini bila ya kujali kile kitakacho mfika wakati anafanya hivyo.

Lissu ambaye ni mbunge kupitia tiketi ya Chadema amesema: “Baadhi ya watu wanafikiria kwamba ninapenda kufungwa jela lakini hilo sio kweli kwa kuwa nina familia na mtoto. Kwa kuwa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia naamini tunahaki ya kueleza maoni yetu na tutaendelea kupigania hilo.

Lissu ambaye pia ni Rais wa Jumuiya ya Mawakili (TLS) amekumbusha siku alipokataa kuchukuliwa mkojo wake ukapimwe.

“Walinichukua toka Kituo cha kati cha polisi kwenda nyumbani kwangu na baada ya kupekuwa nyumba yangu wakaondoka na mimi mpaka kwa Mkemia mkuu wa serikali lakini nilikataa kuchukuliwa kipimo cha mkojo kwa kuwa tuhuma yangu ilikuwa juu ya uchochezi, ambalo wala halihitaji kupimwa mkojo,” amesema Lissu.

Lissu alipewa dhamana na mahakama baada ya kukaa rumande wiki nzima baada ya kukamatwa kwake kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Alhamisi iliyopita wakati alipokuwa anangojea kupanda ndege kuelekea Kigali, Rwanda.

Wakati akitoa dhamana siku ya Alhamisi, Hakimu Wilbard Mshauri, alitupilia mbali hoja ya mwendesha mashtaka, ambapo aliwasilisha kiapo cha kuzuia dhamana ya wakili huyo.

Hakimu alisema kuwa hakuna kumbukumbu yoyote inayoonyesha kuwa Lissu aliwahi kukiuka masharti ya dhamana huko nyuma.

Kadhalika alisema kuwa mawakili 18 waliojitokeza kumwakilisha Lissu ni ushahidi wa kuwa Lissu ni mtu mwenye nafasi yake katika jamii.

Lissu anatuhumiwa na uchochezi baada ya kuhutubia mkutano wa waandishi wa habari Julai 17, ambapo kati ya mambo mengine aliomba jumuiya ya kimataifa kukata misaada kwa uongozi wa Rais Magufuli kama hatua ya kuishinikiza iheshimu misingi ya demokrasia, utawala wa sheria na haki za binadamu.

XS
SM
MD
LG