Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 06, 2022 Local time: 09:48

Makadirio ya kodi kwa Acacia yawashtua wawekezaji Tanzania


Moja ya Machimbo makubwa ya Barrick Gold Mine huko Dominican Republic ambayo inamiliki hisa katika kampuni ya Acacia

Makadirio ya kodi yaliyofanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa kampuni ya Acacia zisipothibitishwa, wadau wanadai kuwa yanaweza kuleta mtikisiko kwa wawekezaji.

Pamoja na nia njema ya Serikali kutaka Taifa linufaike na rasilimali zake, wadau wa biashara ya kimataifa wameonyesha hofu kwamba taarifa zaidi zinahitajika ili kutowatisha wawekezaji wengine wanaotamani kuja nchini.

Vyanzo vya habari nchini Tanzania vimeripoti kuwa Meneja wa Taasisi ya Usimamizi wa Rasilimali (Natural Resources Governance Institute), Kusini na Mashariki mwa Afrika, Silas Olan’g akizungumzia kodi inayodaiwa Acacia alisema tangu sakata la uchunguzi wa sekta ya madini lianze, jamii haijapata taarifa kamili hivyo kila mmoja kuwa na mtazamo wake.

“Makadirio yaliyotolewa na TRA bila shaka yametokana na uchunguzi wao hivyo Acacia nao wanapaswa kutoa taarifa zao. Hilo likifanyika, kila mdau ataweza kufahamu kama kuna mwenye makosa ama la,” alisema Olan’g.

Amesema hilo lisipofanyika na Serikali ikiendelea kukaa kimya: “Italeta mtikisiko kwa wawekezaji walio nje. Taarifa hizi ni muhimu ili kuwa na mtazamo wa pamoja na kuwaondoa woga. Watakaoridhika kwamba Acacia imekiuka mkataba hawatoogopa kuja kuwekeza.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Godfrey Simbeye amesema huenda uamuzi huo umefanywa makusudi ili kuharakisha majadiliano kati ya Serikali na wawekezaji hao.

Ameongeza kuwa TRA imetimiza wajibu wake na ripoti mbili za kamati za uchunguzi zimesaidia kurahisisha tathmini ya kiwango cha kodi ya Acacia ambayo ilitaka kuundwe tume huru, lakini haijafanyika hivyo.

“Kiwango cha kodi kilichokadiriwa ni kikubwa sana na huenda siyo halisi. Hakuna kampuni yenye uwezo wa kulipa fedha hizo labda (tajiri wa kwanza wa dunia) Bill Gates,” alisema Simbeye.

Amesema Acacia wanapaswa kuharakisha mazungumzo ambayo huenda yakapunguza kiasi hicho. “Ubaya ni kwamba hata namna ya kukata rufaa kwa Acacia ni ngumu kwa kuwa watatakiwa kulipa sehemu ya kodi hiyo. Uwezo huo pia hawana,” aliongeza.

Amekumbusha kwamba sakata hilo linatafsiriwa vibaya na wawekezaji wa nje kutokana na sifa mbaya zinazoenezwa na kuifanya Tanzania ionekane ina hatari kubwa kisiasa.

Wakati TRA ikiitaka Acacia kulipa kiasi hicho, taarifa za kampuni hiyo zinasema tangu ianze uzalishaji nchini, imeingiza jumla ya Dola bilioni sita ambazo ni sawa na Sh13.2 trilioni kutokana na mauzo ya dhahabu ya Bulyanhulu na Buzwagi, “Si rahisi kwetu kukwepa kodi kubwa kiasi hicho.”

Licha ya mapato hayo, thamani ya kampuni hiyo ni Dola 1.2 bilioni ambazo ni zaidi ya mara 30 ya kodi inayodaiwa (Dola40 bilioni) na zaidi ya mara 150 ya makadirio yote yanayojumuisha kodi, riba na faini (Dola 190 bilioni).

Wakati baadhi ya wadau wakiwa na shaka juu ya uwezo wa Acacia kulipa deni hilo, Serikali imepongeza hatua zilizochukuliwa na TRA.

“Utaratibu uliotumiwa na TRA ni sahihi. Kama wanaona kiwango ni kikubwa na hawawezi kulipa, taratibu za kukata rufaa kwa kamishna wa kodi zinaeleweka, wazifuate,” alisema Benny Mwaipaja, ofisa habari wa Wizara ya Fedha.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG