Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Oktoba 12, 2024 Local time: 04:10

Kura ya maoni Sudan: Chanzo ni nini?


Rais wa Sudan Omar al-Bashir, kati, akisindikizwa na Makamu Rais Salva Kiir Mayardit, alipowasili uwanja wa Juba Januari 4, 2011 na kuahidi kuunga mkono maamuzi ya Sudan Kusini.
Rais wa Sudan Omar al-Bashir, kati, akisindikizwa na Makamu Rais Salva Kiir Mayardit, alipowasili uwanja wa Juba Januari 4, 2011 na kuahidi kuunga mkono maamuzi ya Sudan Kusini.

Siku ya jumapili, Januari 9 wananchi wa Sudan Kusini wanatarajiwa kushiriki katika zoezi la kura ya maoni ambayo itaamua endapo Sudan kusini itajitenga na Sudan kaskazini au la. Vipi Sudan kusini imefikia hatua hii?

Chanzo ni mkataba wa amani ambao ulisainiwa miaka mitano iliyopita kati ya Sudan kaskazini na kusini, mkataba ambao ulimaliza zaidi ya miongo miwili ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Wachambuzi mbalimbali wa maswala ya siasa wanaupa sifa mpango wa makubaliano ya amani wa Sudan, ambao umemaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyo dumu kwa miongo miwili na kugharimu uhai wa watu zaidi milioni mbili na kuwaacha watu milioni nne bila ya makazi.

Mpango huu, ambao pia umepata nguvu kutoka jumuia ya kimataifa, ulitiwa saini mwaka 2005, kati ya chama cha Sudan People’s Liberation Movement, chenye makao yake Juba, na chama tawala National Congress huko khartoum.

Kati ya mambo mengine, mpango huu wa amani wa Sudan, ulitaka kuondoka kwa vikosi vya kijeshi vya Sudan Kaskazini, huko Sudan Kusini, uchaguzi wa kitaifa, na makubaliano ya kugawana mapato ya mafuta. Vilevile ulitaka kushirikiana madaraka, na kupanga ratiba ya kura ya maoni kwa ajili ya Sudan Kusini kuwa taifa huru.

Baadhi wanasema mpango huu maalum, umefanikiwa kwa baadhi ya ahadi zake. Profesa Emitus Peter Woodward, ambaye anafundisha siasa katika chuo kikuu cha Reading, huko uingereza anasema:

“Pande zote mbili zimeyaona makubaliano kama ni sitisho la mapigano badala ya suluhisho la tofauti zao. Badala ya kukaa pamoja kwenye serikali ya umoja, wameamua kila mtu kwenda upande wake na kuwa na uhusiano mbaya kidogo katika mchakato huo.”

Kuna sababu mbalimbali zinazofanya wachambuzi kusema mpango huu umeshindwa kuhamasisha umoja wa kitaifa.

Wanasema mpango huu, umejali utashi wa pande mbili tu, Chama kilichopo madarakani na chama cha SPLM, lakini umevishirikisha kwa nafasi ndogo vyama vingine na kutoshirikisha eneo la jimbo la magharibi la Dafur.

Vipengele mbalimbali vya mpango huu, havija-jitosheleza ama vingine kuto-jumuishwa. Watu wengi wa Sudan hawajawekewa mazingira bora, na uchambuzi wa mpango huo unasema, serikali imeshindwa kuanzisha tume ya kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu.

Ezekiel Lol Gatkouth, mkuu wa mpango wa Serikali ya Sudan Kusini hapa Washington, anasema:

“Tumeshindwa kuibadili Sudan kuwa sehemu bora kwetu sisi sote. Kwa miaka mitano iliyopita, Sharia, ambayo ni sheria ya Kiislam imekuwepo. Mimi ambaye si mwislam, ninapaswa kuwa katika kundi maalum na tume maalum iliyoanzishwa ili kunilinda na Sharia. Uhuru wa Wanawake umekuwa matatani na wanapigwa pale wanapovaa kinyume na sheria hiyo. Kwa hiyo Sudan imeshindwa kukaa pamoja. Kitu pekee tunachopaswa kufanya kwa sasa, ni kuhakikisha amani haivunjiki na tunaishi kwa amani.”

Wakosoaji wanasema, serikali imeshindwa kufikia lengo lake lililowekwa la kufikia hadi asilimia 30, ya watumishi kutoka Sudan Kusini, na kutambulisha rasimu ya umiliki wa ardhi na kutatua mizozo. Vilevile imeshindwa kutatua migogoro ya mipaka katika eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta la Abyei, lililopo kati ya Sudan Kusini na Kaskazini.

XS
SM
MD
LG