Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Juni 21, 2024 Local time: 21:26

Kikwete avionya vyama tawala Afrika kuachana na kasumba ya uadui


Rais Mstaafu Jakaya Kikwete akimpongeza Rais John Magufuli baada ya kuapishwa kuwa rais.
Rais Mstaafu Jakaya Kikwete akimpongeza Rais John Magufuli baada ya kuapishwa kuwa rais.

Vyama tawala katika Bara la Afrika vimeonywa kuacha kasumba ya kuvichukulia vyama vya upinzani kuwa maadui na badala yake viwaone kama washindani.

Rais mstaafu Jakaya Kikwete wa Tanzania ambaye tangu astaafu baadhi ya wapinzani wamekuwa wakimkumbuka na hata kufuta kumbukumbu za mashtaka ya kufinya demokrasia, kutokana na kile wanachodai kubanwa zaidi na uongozi wa sasa.

Kikwete aliyasema hayo wakati akichangia mada ya Utawala Bora na Utawala wa Sheria iliyowasilishwa na Profesa Barney Pityana, ambaye ni Makamu Mkuu Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Afrika Kusini kwenye Kongamano la Uongozi barani Afrika yaani ‘African Leadership Forum 2017’.

Kikwete aliliambia kongamano hilo la siku mbili lililomalizika Ijumaa Johannesburg nchini Afrika Kusini na kukutanisha viongozi mbalimbali akiwamo mtangulizi wake, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, kuwa vyama tawala viache kasumba ya kuwa upinzani ni maadui kwani huleta chuki na uadui usiokuwa na faida.

Katika hilo, Kikwete alivitaka vyama vya upinzani barani Afrika kutokurudi nyuma katika kunadi sera zao kwa wananchi.

Vyanzo vya habari nchini Afrika Kusini vimesema aliongeza kuwa vyama vya upinzani vinapaswa kuelezea vyema sera zao kwa wafuasi wao ili wazielewe na ufikapo wakati wa uchaguzi wapiga kura wawe na uelewa wa kutosha kuhusu mipango yao ya kuongoza nchi.

Akielezea umuhimu wa vyama vya upinzani katika Taifa lolote lile, Kikwete alisema ni kuvifanya vyama tawala kuwa macho si kulala.

“Pia kazi ya upinzani ni kuiambia Serikali kile inachofanya ni kibaya, ambacho katika chama chako hawawezi kuona au wanaweza kuona lakini wasiwe na ujasiri wa kusema kipi sahihi.

Pamoja na hayo, Kikwete alipongeza baadhi ya nchi ambazo zimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa zinatilia maanani misingi ya utawala bora.

“Si kweli kuwa barani Afrika hakuna utawala wa sheria au kila kitu Afrika ni kibaya hapana. Kumekuwa na juhudi nyingi za kuhakikisha kuwa migogoro inayozikumba baadhi ya nchi inatatuliwa ili kuwe na amani na utulivu katika nchi hizo,” alisema Kikwete.

Kauli hizo za Kikwete zilionekana kumvutia mwanasiasa na kiongozi wa upinzani wa chama cha Democratic Alliance (DA) cha Afrika Kusini, Mmusi Maimane.

Maimane aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa: “Rais Kikwete ameibua hoja ya umuhimu wa upinzani Afrika kama kazi ya utawala bora. Si maadui lakini washindani.”

Hoja hiyo ya Maimane ilimwibua mmoja wa wanasiasa wa upinzani hapa nchini, ambaye pia na mwanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) ambacho kipo kwenye mgogoro mkubwa wa kiuongozi, Ismail Jussa.

Jussa kupitia ukarasa wake wa Twitter aliandika kuwa: “Ni uongo wa hali ya juu, maneno matupu. Ni Kikwete ambaye alituma jeshi kwenda Zanzibar, Oktoba 2015 na kufuta uchaguzi kwa sababu CUF ilikuwa inashinda.”

Akizungumza na wanahabari jana jijini Johannesburg, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, alivitaka vyombo vya habari barani Afrika kuwa wazalendo kwa kuandika habari zitakazosaidia kutatua migogoro na kuleta maendeleo.

Mkutano huo wa siku mbili ulihudhuriwa pia na marais wastaafu Olusegun Obasanjo (Nigeria), Thabo Mbeki (Afrika Kusini), Mohamed Marzouki (Tunisia), Hassan Mohammed (Somalia), Bakili Mulizi (Malawi), Mwanasheria Mkuu wa Uganda, Bart Katureebe.

Ulimalizika jana kwa kuwataka viongozi barani Afrika kuunganisha nguvu zao katika kujenga amani na utulivu barani humo.

################################

XS
SM
MD
LG