Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 29, 2022 Local time: 17:51

Marejeo ya uchaguzi Kenya yaibua kashfa mpya IEBC


Raila na Kenyatta

Mara tu baada ya Wafula Chebukati kuonekana kumtengua Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume hiyo Ezra Chiloba na Maafisa wengine na kuteua wengine saba kuchukua nyadhifa zao, nyaraka za mawasiliano kati ya Chebukati na Chiloba zimeibuka.

Kupitia kwa barua yenye maagizo, Wafula Chebukati anamtaka Chiloba kuelezea bayana kwa nini utambulisho wake wa barua pepe ulitumika kuingia katika seva na kubadilisha matokeo ya kura ya urais.

Pia anatakiwa kuelezea ni kwa nini fomu za uchaguzi hazikuwa na thibitisho la usalama, ni kwa sababu gani simu zenye kima cha shilingi milioni 848 zinazotumia mtandao wa Satellite zilizonunuliwa na tume hiyo hazikutumika.

Kupitia barua hiyo ya Septemba tarehe 5, Chebukati amemtaka Chiloba kueleza ni kwa nini mitambo ya kupeperusha matokeo ya urais kutoka baadhi ya vituo vya maeneo ya bunge kote nchini havikuwa vinapeperusha matokeo halisi. Pia, kuelezea ni kwa nini vituo 595 havikupeperusha matokeo ya urais.

Huku Raila Odinga Kiongozi wa Muungano wa NASA akielezea kuwa waliokuwa wakisema yamethibitishwa kupitia nyaraka hizo.

Wakati tarehe ya uchaguzi wa marudio ya kura ya urais ikiendelea kuonekana kuwa kizungumkuti kati ya chama cha Rais Uhuru Kenyatta na Muungano wa Upinzani unaoongozwa na Raila Odinga, bado vuta nikuvute zinaendelea kushuhudiwa nchini Kenya.

Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa tofauti hizi zimeendelea kushuhudiwa katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka baina ya Mwenyekiti wa Tume hiyo Wafula Chebukati na Afisa Mkuu Mtendaji Ezra Chiloba.

Amesema mgogoro huu pia unaonekana kuwahusisha baadhi ya makamishna ambao wanaonekana kutofurahia uamuzi wa Chebukati kuwatengua baadhi ya maafisa ambao wanasemekana kuhujumu utendaji kazi wa Tume hiyo.

Hata hivyo, Makamishna wa tano wa Tume hiyo ya Uchaguzi wakiongozwa na Naibu Mwenyekiti wa Tume hiyo Consolata Nkatha Maina, Makamishna Yakubu Guliye, Paul Kurgat, Boya Molu na Margaret Mwachanya wamepuuzilia mbali nyaraka hizo na kusema kuwa maagizo yaliyonakiliwa hayakuafikiwa katika vikao vya tume hiyo.

Aidha, Makamishna hao watano wanasema kuwa wamezisoma taarifa hizo kupitia vyombo vya habari kama Wakenya wengine.

Huku hayo yakiendelea, wanasiasa wengi waliobwagwa katika uchaguzi mkuu kutoka vyama tofauti tofauti wameelekea mahakama mbalimbali nchini Kenya kuwasilisha kesi zinazopania kubatilisha ushindi wa viongozi waliochaguliwa katika nyadhifa mbalimbali kabla muda wa kufanya mawasilisho hayo kukamilika.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennedy Wandera Kenya.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG