Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Machi 19, 2024 Local time: 06:57

Shambulizi la Kigaidi Kenya : Majengo yaendelea kupekuliwa, sauti za risasi zasikika


Wafanyakazi wa Red Cross wakimsaidia mwanamke ambaye alifikwa na majonzi baada ya kufahamu kuwa ndugu yake ameuwawa katika shambulizi la kigaidi, Jumatano, Jan. 16 2019, katika jengo la kuhifadhi maiti huko Chiromo Nairobi, Kenya.
Wafanyakazi wa Red Cross wakimsaidia mwanamke ambaye alifikwa na majonzi baada ya kufahamu kuwa ndugu yake ameuwawa katika shambulizi la kigaidi, Jumatano, Jan. 16 2019, katika jengo la kuhifadhi maiti huko Chiromo Nairobi, Kenya.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya Fred Matiangi amesema kuwa kwa sasa vyombo vya usalama vinaendelea kupekuwa hoteli ya Dusit2 na eneo la shambulizi jijini Nairobi ili kutafuta ushahidi.

Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani imeripoti kuwa milio ya risasi ilikuwa inasikika Jumatano asubuhi, katika ghorofa ya saba ya hoteli hiyo ishara kuwa kulikuwa na makabiliano baina ya vyombo vya usalama na magaidi kwa siku ya pili.

Lakini Rais Uhuru Kenyatta amesema Jumatano kuwa watu wenye silaha waliovamia eneo la biashara la hoteli na kuuwa watu 14, “wameuwawa” baada ya takriban masaa ishirini ya mapambano ambapo mamia ya raia waliokolewa.

Wakati huo huo, Marekani na Umoja wa Mataifa zimelaani shambulizi hilo. Msemaji wa idara ya Ulinzi wa Marekani amesema shambulizi hilo ni la kipumbavu huku katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akieleza masikitiko yake juu ya shambulizi hilo la kinyama la kigaidi.

Kwa mujibu wa maofisa wa Kenya kulikuwa na magaidi watano waliouawa na vyombo vya usalama huku mmoja akijitoa mhanga.

"Jengo lote ambalo lilivamiwa sasa ni salama, vyombo vya usalama vimewaokoa idadi kubwa ya wakenya na raia wengine wa kigeni. Tuko kwenye harakati za kukamilisha shughuli hizi,” alisema Waziri wa Mambo ya Ndani.

Rais Uhuru Kenyatta amesema serikali yake itaendelea kuchukua hatua za kuboresha usalama siku za usoni dhidi ya magaidi.

"Tumechukua tahadhari na tuko chonjo, nawahakikishia Wakenya na Wageni ya kwamba mko salama nchini Kenya,” alisema Kenyatta.

Duru za habari zinasema kuwa raia wa Uingereza na Mmarekani ni miongoni mwa watu waliouawa.

XS
SM
MD
LG