Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 01, 2022 Local time: 03:03

Sita wauawa, 30 wajeruhiwa katika shambulizi Kenya


Watu wakijaribu kuondoka eneo la hotel Dusit, Nairobi January 15, 2019.

Watu wasiopungua sita wamefariki na wengine 30 kujeruhiwa na kupelekwa katika hospitali mbali mbali za mjini Nairobi kufuatia shambulizi la kigaidi kwenye hoteli moja ya kifarahari mjini humo Jumanne.

Ripoti zinasema watu watano waliuawa katika mkahawa wa hoteli ya Dusit unaojulikana kama Secret Garden baada ya mshukiwa wa ugaidi kujilipua, kulingana na Inspekta Mkuu wa polisi Kenya Joseph Boinnet.

Mtu mwingine, mwanamke, alifariki kutokana na majeraha yake baada ya kufikishwa katika hospitali ya MP Shah ambayo ilipokea watu sita walioathirika katika shambulizi hilo la Jumanne alasiri.

Watu wanne walionusurika walipekwa katika hospitali ya Aga Khan wakati hospitali ya Kenyatta ilipokea watu wanne wengine waliojeruhiwa.

Shambulizi hilo lilianza kwa mlipuko uliofuatiwa na milio ya risasi katika hoteli ya Dusit katika eneo la Chiromo, mjini Nairobi.

Maafisa wa polisi waliendelea kuwasili katika eneo hilo kwenye barabara ya Riverside Drive. Tukio hilo la mwendo wa saa 3.15 alasiri, lilisababisha msongamano mkubwa kwenye barabara za eneo hilo.

Jumba hilo, ambalo lina hoteli ya kifahari na afisi za kampuni mbalimbali, lilionekana kuzingirwa na maafisa wa kulinda usalama.

Shirika la habari la Al-Jazeera liliripoti kwamba kundi la kigaidi la al-Shabab lilidai kuhusika katika shambulizi hilo.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG