Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 26, 2024 Local time: 09:52

Washambuliaji wote wa 'Dusit2' wameangamizwa - Rais Kenyatta


Shambulizi la Kigaidi lililotokea Nairobi Jumanne tarehe 15 Januari 2109.
Shambulizi la Kigaidi lililotokea Nairobi Jumanne tarehe 15 Januari 2109.

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, amesema Jumatano kwamba operesheni ya kukabiliana na washambuliaji  waliovamia hoteli ya Dusit2 mjini Nairobi imekamilika na kwamba washambuliaji wote "wameangamizwa."

Akihutubia taifa kwa njia mubashara kupitia televisheni kutoka Ikulu, Kenyatta alisifu vyombo vya usalama kwa 'jinsi maafisa walivyo kabiliana na washambuliaji hao na kudhibiti eneo hilo."

Jumanne alasiri, washambuliaji wanaoshukiwa kuwa magaidi waliokuwa wamejihami kwa silaha walivamia jengo la hoteli ya kifahari ya DusitD2 lililo katika mtaa wa Westlands Kilomita chache kutoka katikati ya Jiji la Nairobi na kuua watu wasiopungua 14.

Rais Kenyatta alisema kwamba kufikia wakati alipotoa hotuba yake, watu 14 walikuwa wamepoteza maisha yao katika shambulio hilo na wengine 700 kuokolewa kutoka jengo hilo. Hata hivyo, Shirika la msalaba mwekundu lilinukuliwa na vyombo vya habari likripoti kuwa waliouwawa katika mkasa huo ni watu 24.

Walio jeruhiwa waliendelea kupokea matibabu katika hospitali mbalimbali mjini Nairobi, zikiwemo Agha Khan, Nairobi na Kenyatta.

"Nataka kuwahakikishia Wakenya wote kwamba tutawasaka wote waliohusika katika kufadhili, kupanga na kutekeleza shambulizi hilo popote pale walipo," alisema Kenyatta.

Aidha, rais huyo aliipongeza jumuiya ya kimataifa "kwa kusimama nasi wakati wa mkasa huo."

Kundi la wanamgambo wa Kiislamu la al-Shabab, lilidai kuhusika na shambulio hilo.

Kati ya waliouawa ni raia wa Marekani, ambaye alinusurika katika shambulizi la kigaidi la Septemba 11, 2001. Hayo ni kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani.

Aidha, raia mmoja wa Uingereza pia alifariki katika shambulio hilo.

XS
SM
MD
LG