Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Februari 25, 2024 Local time: 11:43

Kampeni ya CPJ ya kukumbushia siku 500 zakutoweka Azory Gwanda


Azory Gwanda
Azory Gwanda

Kamati ya Kuwalinda Wanahabari (CPJ) Alhamisi imezindua kampeni ya #WhereIsAzory kukumbushia suala la mwandishi wa habari wa kujitegemea Mtanzania Azory Gwanda, ambapo kesho zitatimia siku 500 toka alipoonekana mara ya mwisho.

Kampeni hiyo inalenga kuhamasisha, kujenga uelewa kuhusu Gwanda, na kuzitaka mamlaka za Tanzania kufanya uchunguzi wa kuaminika na kuweka bayana hatma yake.

Watu wanaweza kushiriki katika kampeni kwa kutumia hashtag #WhereIsAzory na #MrudisheniAzory katika mitandao ya kijamii.

“Azory Gwanda ni mwandishi wa habari wa kujitegemea aliyekuwa akiandika kuhusu jamii yake na kamwe hapaswi kuwa takwimu nyingine tu,” anasema Angela Quintal, mratibu wa CPJ Afrika.

“Kupitia kampeni hii tunataka kuhakikisha kwamba kesi ya Gwanda inapewa kipaumbele na mamlaka za Tanzania na kupata majibu yanayohitajika kuhusu kile hasa kilichompata. Mpaka wakati huo, waandishi wa Tanzania hawawezi kujisikia wako salama.”

Mara ya mwisho Gwanda kuonana na familia yake na rafiki zake ilikuwa Novemba 21, 2017, kwa mujibu wa utafiti wa CPJ. Gwanda alimuambia mkewe, Anna Pinoni, kwamba ana safari ya dharura na angerejea siku inayofuata.

Hajaonekana tangu siku hiyo. Katika mahojiano na gazeti la Mwananchi , Pinoni alisema anadhani kupotea kwa mume wake kunaweza kuhusishwa na kazi yake ya kuripoti juu ya mfululizo wa mauaji ya ajabu yaliyokuwa yakitokea katika mkoa wa Pwani nchini Tanzania, maoni yanayoshikiliwa na wengine ambao CPJ iliongea nao.

Nchini Tanzania, waandishi wa habari na vyombo vya habari wanachukua tahadhari kwa kuhofia yanayoweza kuwakuta iwapo watapaza sauti kuhusu kesi ya Gwanda.

Wakati wawakilishi wawili wa CPJ waliposhikiliwa kwa usiku mmoja na kuhojiwa nchini Tanzania mwaka uliopita, waliulizwa juu ya maslahi yao katika kisa cha Gwanda.

Kupotea kwake kunakuja huku kukiwa na kuzorota kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini, ikiwa ni pamoja na maagizo ya serikali kufungia baadhi ya vyombo vya habari, faini, kanuni zenye vizuizi na kukamatwa hovyo kwa waandishi wa habari.

CPJ Afrika itaangazia kesi ya Gwanda katika Twitter, Facebook, na Instagram. ### CPJ ni kamati huru, isiyojiendesha kwa faida inayofanya kazi kulinda uhuru wa wanahabari duniani kote.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.


XS
SM
MD
LG