Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Februari 23, 2024 Local time: 21:18

Kagame amteua Waziri Mkuu mpya Rwanda


Paul Kagame apokea ngao kama ni alama ya kukabidhiwa uongozi baada ya kuapishwa kuwa rais wa Rwanda
Paul Kagame apokea ngao kama ni alama ya kukabidhiwa uongozi baada ya kuapishwa kuwa rais wa Rwanda

Rais Paul Kagame wa Rwanda Jumatano amemteua waziri mkuu mpya.

Uteuzi huo wa Dr Eduard Ngirente unakuja siku 13 baada ya Rais Kagame kula kiapo cha kuliongoza taifa kwa awamu nyingine.

Rais Kagame aliapishwa Agosti 18 kufuatia ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi wa Agosti 04 mwaka huu.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA anaripoti kuwa zoezi hilo la uteuzi limefanyika kwenye jengo la bunge mjini Kigali jioni ya leo likiongozwa na Rais Paul Kagame.

Waziri Mkuu mpya Dr Ngirente mwenye umri wa miaka 44 na mwanauchumi kitaaluma anarithi kiti hicho kutoka kwa Anastase Murekezi aliyekalia kiti hicho tangu mwezi Julai mwaka 2014.

Rais Paul Kagame amesema: "Tumempata waziri mkuu mpya ambaye ataongoza baraza la mawaziri nimepata wakati wa kutosha kuzungumza naye, na tumekubaaliana jinsi tutakavyoshirikiana naye kutekeleza majukumu haya mapya ambayo ni ya kawaida. Ila zaidi nimemwambia kwamba atafanya kazi kwa kushirikiana na watu wengine ambao ni binadamu."

Rais Kagame ameahidi kuwa Jumatano jioni wananchi watatangaziwa baraza jipya la mawaziri. Ameongeza kuwa kesho mawaziri wapya wataapishwa, huku akidokeza kuwa mawaziri wanawake wataongezeka na pengine kuvuka asilimia 30 inayoainishwa na katiba ya Jamhuri ya Rwanda.

"Sasa kinachofuata ni baraza la mawaziri ambalo pengine mtalipata jioni hii,baraza ambalo tumehakikisha wananchi wote wa Rwanda watawakilishwa kwenye baraza hilo.Lakini pia hii ni kwa mujibu wa katiba kama mnavyojua, kuna wale wataoachwa na kutakuwa na damu mpya lakini ni jambo la kawaida mnalojua," ameongeza Kagame.

Katiba ya Rwanda inamtaka Rais kumtangaza Waziri ndani ya kipindi kisichozidi siku 15 tangu kula kiapo

Waziri Mkuu mpya, Eduard Ngirente hajulikani sana katika siasa za Rwanda na kabla ya uteuzi wake, aliwahi kutumikia wizara ya Fedha na Mipango ya Kiuchumi akiwa mshauri wa waziri kabla ya kuhamia Benki ya Dunia alikohudumu kama mshauri wa masuala ya kiuchumi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, jijini Washington Dc tangu mwaka 2014 hadi alipoteuliwa kwenye wadhifa wa waziri mkuu.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Sylivabus Karemera, Rwanda

XS
SM
MD
LG