Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Machi 19, 2024 Local time: 05:46

Jenerali wa zamani wa Burundi Ndayirukiye afariki gerezani


Cyrille Ndayirukiye
Cyrille Ndayirukiye

Jenerali wa zamani wa jeshi la Burundi Cyrille Ndayirukiye ambaye alikuwa anatumikia kifungo cha maisha jela kwa shutma za kujaribu kuuangusha utawala wa hayati rais Pierre Nkurunziza wa Burundi amefariki Jumamosi.

Ndayirukiye aliyehukumiwa tarehe 13 Mei 2015, aliaga dunia akiwa katika gereza la mkoa wa Gitega, katikati mwa Burundi, vyanzo vya habari nchini humo vimesema.

Kwa mujibu wa gazeti huru la mtandaoni, Iwacu, Jenerali Ndayirukiye amepatwa na kifo cha gafla. “ Alikuwa anamaliza kuanika nguo zake alizokuwa amezifua mwenyewe alipopatwa na kizunguzungu. Lakini hakuanguka chini, mfungwa mwenzake alimshika mkono asianguke,” taarifa ya Iwacu imesema, ikimnukuu mfungwa huyo.

“Lakini mara tu, sehemu ya mwili wake ulipooza, na hakuamuka tena. Alifariki kati ya saa tisa na nusu na saa tisa na dakika 40 alasiri”, chanzo cha Iwacu kimeongeza.

Maafisa wa serikali ya Burundi, walikua hawajatoa taarifa kuhusu kifo chake. Mtandao mwengine wa habari “SOS media Burundi, nao pia umethibitisha kifo cha Jenerali huyo.

Cyrille Ndayirukiye alikua miongoni mwa maafisa wa jeshi waliongoza jaribio la kutaka kumuondoa madarakani rais wa zamani wa Burundi Pierre Nkurunziza, tarehe 13 Mei, 2015, ambae wakati huo alikua jijini Dar es Salaam kushiriki mkutano wa kilele wa ma rais wa nchi wanachama wa jamuia ya Afrika mashariki.

Jaribio hilo lilizimwa na wanajeshi watiifu kwa Nkurunziza. Ndayirukiye na wenzake wa tatu walijisalimisha asubuhi ya tarehe 14 Mei.

Jenerali Ndayirukiye, ambaye aliwahi kuwa waziri wa ulinzi kati ya 2000 na 2002 amefariki dunia akitumikia hukumu ya kifungo cha maisha jela, alichopewa na mahakama ya juu ya Burundi.

Burundi iliingia katika mzozo mbaya wa kisiasa tangu Mei 2015. Mamia ya wafuasi wa upinzani walioshiriki maandamano ya kupinga muhula wa tatu wa rais wa wakati huo Pierre Nkurunziza, inadaiwa waliuawa, na maelfu ya wengine kufungwa jela, huku zaidi ya watu 400,000 wakikimbilia katika nchi jirani.

XS
SM
MD
LG