Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Machi 28, 2024 Local time: 12:30

Rais wa zamani wa Burundi ahukumiwa maisha gerezani


Rais wa zamani wa Burundi Pierre Buyoya
Rais wa zamani wa Burundi Pierre Buyoya

Mahakama kuu nchini Burundi imemhukumu aliyekuwa rais wa nchi hiyo Pierre Buyoya kifungo cha maisha gerezani bila yeye kuwepo mahakamani.

Buyoya amehukumiwa pamoja na watu wengine 18 kwa madai ya kuhusika katika mauaji ya aliyekuwa rais wa kwanza wa Burundi kuchaguliwa kwa njia ya demokrasia Melchoir Ndadaye.

Kulingana na mahakama, 19 hao wamepatikana na makosa ya kushambulia kiongozi wa nchi, na kujaribu kusababisha machafuko, mapigano na mauaji ya halaiki ya watu nchini Burundi.

Mashtaka dhidi ya aliyekuwa waziri mkuu Antoine Nduwayo yamefutwa baada ya ushahidi dhidi yake wa kushiriki katika njama hiyo, kukosekana.

Buyoya, ambaye sasa anafanya kazi kama mwakilishi maalum na kiongozi wa ujumbe wa amani wa kimataifa unaongozwa na Afrika - AFISMA, nchini Mali, amekuwa akitafutwa na mamlaka nchini Burundi baada ya kibali cha kimataifa kutaka akamatwe na kupelekwa nchini humo kutolewa mnamo mwaka 2018.

Kibali hicho cha kukamatwa kilitolewa na mwanasheria mkuu wa Burundi Sylvestre Nyandwi, kwa kushukiwa kupanga njama za kumuua rais wa kwanza kutoka jamii ya Hutu, Ndadaye.

Buyoya, ambaye anatoka jamii ya watutsi, ametaja mashtaka dhidi yake kuwa mbinu ya kugawanya nchi na kubadili mawazo ya watu kutokana na matatizo yanayoikumba nchi hiyo.

Ndadaye aliuawa Oktoba 21 1993, siku 102 baada ya kuapishwa kuwa rais wa Burundi.

Machafuko ya kikabila yalitokea Burundi kufuatia mauaji ya Ndadaye na kupelekea vifo vya watu 300,000 miaka miwili baada ya kusainiwa

kwa mkataba wa umoja kati ya makabila ya Hutu, Tutsi na Twa, Februari 5 1991.

Mauaji ya Melchoir Ndadaye ni swala ambalo limekuwa likizungumziwa sana wakati wa makumbusho ya kifo chake, jamii ya Hutu ikitaka haki itendeke.

Baadhi ya wanajeshi wa ngazi ya chini walipatikana na hatia mwaka 1999 na kuhukumiwa, lakini baadhi ya watu nchini Burundi wana maoni kwamba haki haijatendeka.

Mnamo Desemba mwaka 2018, serikali ilikamatwa maafisa wa jeshi wanne wa ngazi ya juu na raia mmoja kuhusiana na mauaji hayo, na kutoa kibali cha kimataifa kutaka washukiwa wengine wote wakamatwe na kushitakiwa.

Wengi wa washukiwa kwenye orodha hiyo ni wanajeshi wastaafu na waliokuwa maafisa katika chama chenye Watutsi wengi cha Uprona, na wengi wao wanaishi katika nchi jirani ya Rwanda na Ubelgiji.

Ubelgiji ni mkoloni wa Burundi.

-Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG