Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 28, 2025 Local time: 09:13

Jamhuri ya Afrika ya Kati yapiga kura ya maoni kuhusu kubadilisha katiba


Rais Faustin Archange Touadera (Katikati) apiga kura ya maoni katika shule ya sekondari ya Boganda mjini Bangui, Julai 30, 2023.
Rais Faustin Archange Touadera (Katikati) apiga kura ya maoni katika shule ya sekondari ya Boganda mjini Bangui, Julai 30, 2023.

Jamhuri ya Afrika ya Kati inapiga kura ya maoni ya katiba leo Jumapili ambayo iwapo itapitishwa inaweza kuondoa ukomo wa muhula wa urais, na kumruhusu Rais Faustin-Archange Touadera kuwania muhula wa tatu hapo mwaka 2025.

Touadera alichaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2016 kwa muhula wa miaka mitano, na alichaguliwa tena mnamo mwaka 2020 kwa kile ambacho kilipaswa kuwa muhula wake wa mwisho madarakani.

Katiba mpya itabadilisha hali hiyo, ikimruhusu kugombea muhula mpya wa miaka saba, na idadi ya mihula ambayo yeye au mgombea mwingine anaweza kuwania urais itakuwa isiyo na kikomo.

Vyama vya upinzani na baadhi ya mashirika ya kiraia yametoa wito wa kususia kura hiyo ya maoni, vikisema kuwa iliandaliwa kumuweka Touadera madarakani maisha yake yote.

Idadi ya wapiga kura walikuwa wachache katika kituo kimoja cha kupigia kura katika kitongoji cha kaskazini mwa mji mkuu Bangui mapema Jumapili, kikiwa na wapiga kura wapatao dazeni mbili kwenye foleni, kulingana na ripota wa shirika la habari la Reuters.

"Nina matumaini kwamba marafiki zangu watajitokeza kwa wingi kupiga kura. Ninachotaka sana ni utulivu ili nchi iendelee," alisema Laurent Ngombe, mwalimu na mmoja wa watu wa kwanza kupiga kura.

Nchi hiyo, inayotoshana na Ufaransa kwa ukubwa, na yenye wakazi karibu milioni 5.5, ina madini mengi zikiwemo dhahabu, almasi na mbao. Imeshuhudia msururu wa ukosefu wa utulivu, ikiwa ni pamoja na mapinduzi na uasi, tangu kupata uhuru kutoka kwa Ufaransa mnamo mwaka 1960.

Touadera, mwenye umri wa miaka 66, mtaalam wa hesabu, amejitahidi kuzima vikundi vya waasi ambavyo vimedhibiti maeneo kadhaa ya nchi tangu Rais wa zamani Francois Bozize, kuondolewa madarakani na uasi mwingine hapo mwaka 2013.

Touadera aliigeukia Russia kwa usaidizi wa kukabiliana na waasi hapo mwaka 2018. Tangu wakati huo, zaidi ya wanajeshi 1,500, wakiwemo wakufunzi na wanakandarasi binafsi wa kijeshi kutoka kundi la Wagner la Russia, wametumwa nchini humo kushirikiana na jeshi la taifa.

Forum

XS
SM
MD
LG