Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Novemba 30, 2022 Local time: 14:33

Mahakama Kuu Tanzania : Jaji ashangazwa na kucheleweshwa kwa dhamana ya Mbowe na Matiko, awapa dhamana


Freeman Mbowe na Ester Matiku

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Alhamisi imetengua uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wa kuwafutia dhamana Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini wa chama hicho, Ester Matiko.

Mahakama hiyo imekubali maombi yao ya dhamana ikiwa ni pamoja na kuripoti mahakamani mara moja kwa mwezi badala ya polisi kila wiki, imeripoti Global Publishers nchini Tanzania.

“Hii ni rufaa mojawapo ambayo sijawahi kuiona katika kazi yangu ya ujaji. Maofisa wa mahakama kama mahakimu wanapaswa kutumia utashi wao kuamua haki za watu kwa kuzingatia haki maana ni hatari sana kumnyima dhamana mtu bila sababu za msingi,” alisema Jaji Sam Rumanyika.

“Kuanzia sasa, naagiza Mbowe na Matiko waachiwe huru mara moja na watatakiwa kuripoti mahakamani mara moja kwa mwezi badala ya polisi kila wiki," ameongeza.

Wakati wa hukumu hiyo iliyotolewa na Jaji Rumanyika, ulinzi mahakamani hapo ulikuwa umeimarishwa kwa askari wengi waliotanda sehemu mbalimbali.

Jaji Wilbard Mashauri akiwa Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Novemba 23, 2018, alifuta dhamana ya Mbowe na Matiko kutokana na kukiuka masharti ya dhamana.

Kufuatia hilo washtakiwa walikata rufaa katika Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga uamuzi wa Mahakama ya Kisutu kufuta dhamana yao ambapo rufani yao ilipangwa kusikilizwa na Jaji Rumanyika.

Hata hivyo, baada ya Mahakama Kuu chini ya Jaji Rumanyika kusikiliza mapingamizi ya pande zote, iliamua kuanza usikilizaji wa rufaa hiyo.

Upande wa serikali ukiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Paul Kadushi, ulidai kuwa wamekata rufaa katika Mahakama ya Rufani kupinga maamuzi yaliyotolewa na Mahakama Kuu.

Hata hivyo, Machi 1, 2019, Mahakama ya Rufaa chini ya jopo la majaji watatu: Stella Mugasha, Dk Gerald Ndika na Mwanaisha Kwariko, ilitupilia mbali pingamizi hilo la serikali na kuamuru kesi hiyo irudishwe Mahakama Kuu kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Washington, DC.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG