Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Februari 01, 2023 Local time: 16:12

ICC yataka Bashir na wenzake kufunguliwa mashtaka kwa haraka


Rais Omar al-Bashir alipokuwa anawasili mahakamani mjini Khartoum, July 21, 2020.

Mwendesha mashtaka wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu-ICC, Fatou Bensouda alisema Jumanne alijadiliana na maafisa wa Sudan kuwapa fursa wachunguzi kufuatilia mashtaka ya ukatili unaodaiwa kufanywa katika mkoa wa Darfur chini ya rais aliyeondolewa madarakani Omar al-Bashir.

Wakati huohuo Bensouda, alisema Rais Omar al-Bashir aliyeondolewa madarakani pamoja na washukiwa wengine wanaotafutwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu kwa shutuma za uhalifu wa vita na mauaji ya halaiki huko Darfur lazima wakabiliwe na sheria bila kucheleweshwa zaidi.

Bashir ambaye aliondolewa madarakani April mwaka 2019 amekuwa akitakiwa na mahakama ya ICC kwa takribani muongo mmoja kwa mashtaka ya mauaji ya halaiki, uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya binadamu katika mkoa wa magharibi wa Darfur.

Njia za kuwashitaki watuhumiwa inajumuisha kesi kuendeshwa nchini Sudan pamoja na mahakama maalum, zilijadiliwa na viongozi wa Sudan, mwendesha mashtaka Bensouda aliwaambia waandishi wa Habari Jumanne jioni wakati wa ziara mjini Khartoum.

Bensouda, mwendesha mashtaka wa ICC, anaeleza : "Kuhusu njia hizo, mamlaka ya Sudan wamenijulisha kwamba wanaangalia mambo kadhaa pamoja na kesi yenyewe kusikilizwa Sudan, ikijumuisha chaguo jingine la mahakama ya mchanganyiko au mahakama maalumu. Haya ni baadhi ya mambo ambayo wanafikiria, ambayo tumeyazungumzia."

Bensouda anaongoza ujumbe wa ICC ambao umekuwepo Khartoum tangu Jumamosi kwa kazi ya kutathmini njia za kuwawajibisha Bashir na wengine wanaohusika na mzozo wa Darfur, ambao ulisababisha maelfu ya watu kufa.

Bensouda anafafanua : "Lazima sasa tufuate na kutekeleza ahadi ya majadiliano ya wiki hii kwa hatua madhubuti. Waraka wa maelewano juu ya njia za ushirikiano, ziara ya kiufundi na fursa ya haraka kwenda Sudan kwa wachunguzi wetu vilijadiliwa.

Mwendesha mashtaka wa ICC, alisifu juhudi za ushirikiano zinazofanywa na maafisa wa mpito wa Sudan ambao walichukua madaraka baada ya kuondolewa kwa Bashir, na kuelezea ziara yake nchini Sudan kuwa ya kihistoria.

Alisema kuwa anataka kufungua uchunguzi nchini humo kuhusiana na Darfur haraka iwezekanavyo. Bensouda pia alielezea matumaini ya kutuma ujumbe wa kudumu nchini Sudan, na akasema alijadili suala hilo na maafisa huko.

Bensouda ameongeza kuwa : "Tunafanya kazi kwa bidi sana na wachunguzi, tumeomba uchunguzi wetu ufanyike hapa nchini haraka iwezekanavyo.

ICC ina hati za kumkamata Bashir na washukiwa watatu wengine wa Sudan, kwa tuhuma za mashtaka ya uhalifu wa vita, mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya binadamu. Akiwemo aliyekuwa gavana wa Kordofan Kusini, Ahmed Haroun na waziri wa zamani wa ulinzi Abdelrahim Mohamed Hussein. Wote wawili wapo chini ya ulinzi nchini Sudan.

Mtu wa tano, kiongozi wa waasi Abdallah Banda, anatafutwa na ICC lakini amekimbia.

Mapigano huko Darfur yalizuka mwaka 2003 kati ya waasi walio wachache wa kiafrika, wakilalamika kutengwa kwa eneo hilo, na vikosi vinavyoungwa mkono na serikali.

Umoja wa Mataifa unakadiria mapigano hayo yaliuwa watu laki tatu na wengine milioni 2.5 walikoseshwa makazi yao.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG