Zaidi ya darzeni ya wanajeshi walioasi walijitokeza kwenye televisheni ya taifa Jumatatu kutangaza na wamesema mapinduzi hayo yamefanyika bila ya ghasia.
Kapteni Sidsore Kaber Ouedraogo alisema viongozi wapya wa kijeshi wataandaa tarehe “itakayo kubalika na kila mtu” ya kufanyika uchaguzi mpya.
Hatua hii inafuatia taarifa za kuwepo mapigano makali karibu na kasri ya rais katika mji mkuu, Ouagadougou.
Hivi sasa haiko bayana mahali aliko Kabore. Ripoti za awali Jumatatu zilisema anashikiliwa na wanajeshi walioasi pamoja na viongozi wengine katika serikali yake.
Tangazo lililosainiwa na Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba limesema Jumatatu kuwa wale wanaoshikiliwa wako katika sehemu salama.
Taarifa hiyo imemlaumu Kabore kwa kushindwa kuliunganisha taifa na kusema hakuwa na weledi wa kukabiliana na changamoto zinazolikabili taifa hilo.
Chama cha Kabore kimesema mapema kuwa alinusurika katika jaribio la mapinduzilakini halikutoa maelezo zaidi.
Burkina Faso imeingia katika vita dhidi ya makundi ya kigaidi yenye uhusiano na al-Qaida na Islamic State tangu mwaka 2015. Uvumi juu ya mapinduzi umeendelea kwa wiki kadhaa baada ya kituo cha kijeshi kaskazini mwa nchi hiyo kuvamiwa na magaidi, na kuwaua wanajeshi 49.
Rais Kabore aliwafukuza kazi mawaziri katika baraza lake na viongozi wa kijeshi mwezi Disemba kufuatia shambulizi hilo.
Ghasia hizi za sasa zilianza mapema Jumapili wakati silaha nzito ziliposikika ndani ya kambi kubwa ya kijeshi mjini Ouagadougou, kambi ya Sangoule Lamizana.
Mwandishi wa habari wa VOA Henry Wilkins alishikiliwa ndani ya kambi kwa muda na kuzungumza na mmoja wa walioandaa uasi, akiorodhesha madai yao hao waliofanya mapinduzi ikiwemo “fedha zaidi na wanajeshi zaidi” kusaidia katika vita dhidi vya ugaidi, na pia kupatiwa mafunzo bora zaidi na kuandaa kikosi cha kijeshi cha kudumu katika mstari wa mbele.
Waliofanya mapinduzi pia wametaka kujiuzulu kwa kiongozi mkuu wamajeshi na mkuu wa usalama, na pia huduma bora kwa waliojeruhiwa na familia za wanajeshi waliokufa katika vita hivyo.
Mapinduzi hayo yaliyotokea nchini Burkina Faso ni ya tatu katika Afrika Magharibi katika kipindi cha miezi 18, kufuatia yale ya Mali na nchi jirani ya Guinea.
Baadhi ya Habari hizi zinatokana na vyanzo vya mashirika ya habari ya The Associated Press, Reuters and Agence France-Presse.