Wito huu unatolewa baada ya mapigano kuongezeka katika jimbo la Tigray kulingana na maafisa wa Umoja wa Afrika.
Mwenyekiti wa Tume ya AU Moussa Faki Mahamat ameeleza "wasi wasi wake mkubwa" kuhusu kuongezeka kwa mapigano hayo na kutoa wito wa kusitishwa mara moja bila ya masharti mapigano na kuanza tena huduma za dharura katika maeneo yaliyotengwa kutokana na mapigano.
Mji wa Shire kaskazini magharibi mwa Tigray umeshambuliwa kwa mabomu mnamo siku chache zilizopita kutokana na mapigano ya pamoja yanayofanywa na wanajeshi wa Ethiopia na Eritrea dhidi ya wapiganaji wa jimbo hilo.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameongeza sauti yake kwa wito uliotolewa na Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi unaonya juu ya kuongezeka kwa mapigano na idadi ya majeruhi miongoni mwa raia, na kutoa wito kwa pande zote kusitisha ugomvi unaosababisha maafa makubwa.
Serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed na maafisa wa Tigray wamekubali mualiko wa mazungumzo kutoka AU, lakini majadiliano yaliyopangwa kuanza mwishoni mwa wiki iliyopita huko Afrika Kusini hayajaanza na hakuna tarehe mpya iliyopangwa.
Getachew Reda msemaji wa kundi la wapiganaji wa Tigray, TPLF amepongeza taarifa ya AU, “kutokana na mzozo wa kutisha wa kibinadamu unaojitokeza kwasababu ya mashambulizi ya jeshi la Eritrea na washirika wake wa Ethiopia.”
Mazungumzo ya upatanishi yalikua yaongozwe na mjumbe wa AU kwa Pembe mwa Afrika Olusegun Obasanjo, makamu rais wa zamani wa Afrika Kusini Phumzile Mlambo-Ngcuka na rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta.