Makundi yenye silaha nchini Libya yalipigana katika viunga vya magharibi mwa Tripoli Ijumaa jioni na mapema Jumamosi wakati vikosi vilivyoshirikiana na serikali ya Abdulhamid al Dbeibah vikiimarisha udhibiti wao juu ya mji mkuu.
Mapigano yametokea huko Warshafala wilaya ya magharibi mwa Tripoli ambayo imekuwa eneo la mapigano ya mara kwa mara katika kipindi chote cha miaka 11 ya ghasia na machafuko tangu uasi ulioungwa mkono na NATO uliopelekea kuondolewa madarakani kiongozi wa muda mrefu Muammar Ghaddafi.
Mapigano hayo pamoja na kundi kubwa linalomuunga mkono Dbeibah kuchukua makao makuu ya kijeshi kusini mwa Tripoli yanakuja wiki moja baada ya pambano kubwa zaidi la vita nchini Libya kwa miaka miwili huku makundi kadhaa hasimu yakipigana ndani na nje ya mji mkuu.