Mji mkuu wa Libya ulikuwa kimya mapema Jumapili, siku moja baada ya mapigano mabaya sana kutokea kwa miaka miwili na kuua watu 32 na kujeruhi 159 huku vikosi vilivyofungamana na utawala unaoungwa mkono na bunge vikishindwa kuiondoa serikali yenye makao yake mjini Tripoli.
Barabara katika jiji hilo zilikuwa na watu wengi kwenye magari, maduka yalikuwa wazi, na watu walikuwa wakiondoa vioo vilivyovunjwa na kusafisha uchafu mwingine kutokana na ghasia za Jumamosi, huku magari yaliyoteketea kwa moto yakiwa yametanda katika baadhi ya mitaa katikati ya mji wa Tripoli.
Mapigano hayo yameibua hofu ya kutokea mzozo mkubwa nchini Libya kutokana na mivutano ya kisiasa kati ya Waziri Mkuu Abdulhamid al-Dbeibah mjini Tripoli na Fathi Bashagha, ambaye anataka kusimika serikali mpya katika mji mkuu.
Jaribio la Bashagha siku ya Jumamosi kuchukua mikoba mjini Tripoli lilikuwa ni jaribio lake la pili tangu mwezi Mei.
Hata hivyo, mashirika ya ndege yalisema mapema Jumapili kwamba safari za ndege zilikuwa zikifanya kazi kama kawaida katika uwanja wa ndege wa Mitiga mjini Tripoli, ikiwa ni ishara kwamba hali ya usalama imerejea kwa sasa.