Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Mei 05, 2024 Local time: 18:07

Mzozo wa Israel na Hamas watawala mkutano wa NAM Kampala


Viongozi wa nchi zisizofungamana na upande wowote (NAM) waliohudhuria mkutano wa 19 wa jumuiya hiyo huko Kampala Uganda Januari 19, 2024. Picha na REUTERS/Abubaker Lubowa
Viongozi wa nchi zisizofungamana na upande wowote (NAM) waliohudhuria mkutano wa 19 wa jumuiya hiyo huko Kampala Uganda Januari 19, 2024. Picha na REUTERS/Abubaker Lubowa

Mzozo wa Israel na wanamgambo wa Hamas ulitawala katika hotuba za viongozi wa nchi wanachama wa mataifa yasiyofungamana na upande wowote yaani Non-Aligned Movement (NAM) katika kongamano la 19 la Vuguvugu hilo lililofanyika Kampala, Uganda.

Kiongozi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Dennis Francis amewaambia viongozi ambao wanahudhuria mkutano wa 19 wa NAM jijini Kampala kwamba anasikitishwa na maafa yanayoongezeka huko Ukanda wa Gaza na kutaka vita kati ya Israel na Hamas visitishwe.

Katika hotuba yake kwenye kongamano hilo la wakuu wa nchi na serikali, Francis alitoa wito kwa Vuguvugu hilo kutumia ushawishi wake na kukomesha mauaji yanayoshuhudiwa kila siku katika Ukanda wa Gaza.

“Nitaunga mkono na kuhimiza mipango yoyote ya kuleta usalama na kutetea haki za binadamu’ pia, natoa wito kwa viongozi wa Vuguvugu hili kuonyesha ushawishi wao katika kukomesha mauaji ambayo tunashuhudia katika ukanda wa Gaza’’ Francis alisema.

Moshi ukifuka angali huko Gaza Januari 18,2024
Moshi ukifuka angali huko Gaza Januari 18,2024

Katika halfa hiyo, Umoja wa Afrika pia ulilaani mashambulizi ya kijeshi yanayotekelezwa na Israel huko Gaza ambapo Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Mousa Faki Mahamat alisema mashambulizi hayo hayakubaliki na yana kiuka haki za binadamu na kutaka vita hivyo dhidi ya Wapalestina kusitishwa mara moja.

Mahamat aliongeza kuwa, watu wa Palestina wana “uungaji mkono kamili na usioyumba’’ wa AU.

“Afrika inalaani vita vya Gaza na inataka visitishwe mara moja kwasababu, siyo vya haki na vinakiuka haki za binadamu. Kama NAM, sote tunapaswa kusimama kidete na kulazimisha haki ya kimataifa na sheria za kimataifa kwa watu wote wanaopigania uhuru.”

Mahamat alisema hayo muda mfupi baada ya Uganda chini ya uongozi wa Rais Yoweri Museveni kuchukua rasmi wadhifa wa uenyekiti wa zamu wa miaka mitatu wa Vuguvugu hilo, kundi kubwa zaidi la mataifa duniani baada ya Umoja wa Mataifa.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni akikabidhiwa wadhifa wa uwenyekiti wa jumuiya hiyo
Rais wa Uganda Yoweri Museveni akikabidhiwa wadhifa wa uwenyekiti wa jumuiya hiyo

Israel ilianzisha mashambulizi yake huko Gaza kujibu shambulizi la Hamas Oktoba 7, 2023 ambalo liliripotiwa kusababisha vifo vya zaidi ya watu 1200. Tangu wakati huo, zaidi ya watu 24,000 wengi wao wanwake na watoto, wameuawa huko Gaza kulingana na wizara ya afya inayomilikiwa na Hamas

Hamas iliorodheshwa kama kundi la kigaidi na Israel na mataifa mengi ya Magharibi ikiwemo Marekani.

Mkutano huo ambao ulianza tarehe 15 Januari 2024 jijini Kampala ulianza na hotuba za wawakilishi wa mataifa wanachama ambapo Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini Grace Naledi Mandisa Pandor aliyaomba mataifa wanachama kuunga mkono kesi iliyowasilishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) dhidi ya Israel, kwa madai ya kutekeleza mauaji ya kimbari ampapo mataifa hayo yaliunga mkono hoja hiyo.

Mkutano huo wa kilele wa siku tano ulianza Jumatatu chini ya kauli mbiu: ‘’Kukuza Ushirikiano kwa Ustawi wa Pamoja wa Kimataifa’’.

Imetayarishwa na Sadam Muballe, VOA Kampala, Uganda.

Forum

XS
SM
MD
LG