Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Oktoba 03, 2023 Local time: 20:38

Zimbabwe: Muda wa kupiga kura waongezewa hadi Alhamisi katika vituo kadhaa


General election in Zimbabwe

Maafisa wa uchaguzi nchini Zimbabwe, waliongeza muda wa upigaji kura katika uchaguzi wa rais hadi Alhamisi, baada ya kucheleweshwa kwa hadi saa 10 katika ngome nyingi za upinzani.

Hayo yalijiri wakati Rais Emmerson Mnangagwa akitafuta muhula wa pili na wa mwisho katika nchi yenye historia ya uchaguzi wenye ghasia na utata.

Visa vya fujo viliripotiwa katika baadhi ya vituo vya kupigia kura nchini humo, huku karatasi za kupigia kura ambazo zilichelewa kuwasilishwa kwa hadi saa 10, zikiisha, na kuwalazimu maafisa kusimamisha zoezi hilo, majira ya usiku wa kuamkia leo, katika vituo vingi, hasa katika maeneo ya mijini ukiwemo mji mkuu wa Harare.

Baadhi ya wapiga kura walisubiri zoezi hilo kwa saa nyingi, wakisema walikuwa na matumaini ya mabadiliko ya kiuchumi, lakini wachambuzi walikuwa na mashaka, iwapo chama tawala cha ZANU-PF, kingeruhusu uchaguzi wa kuaminika, au kuachia madarakani.

Rais Emmerson Mnangagwa anagombea tena, baada ya muhula wa kwanza ambapo mfumuko wa bei, uhaba wa fedha na ukosefu wa ajira, ulisababisha Wazimbabwe wengi kutegemea fedha kutoka kwa jamaa zao nje ya nchi, ili kujikimu kimaisha.

Mnangagwa, mwenye umri wa miaka 80, alichukua wadhifa huo wakati kiongozi wa muda mrefu Robert Mugabe alipoondolewa katika mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2017. Rais Mnangagwa anamenyana na wagombea wengine 10, akiwemo mpinzani wake mkuu, wakili na mchungaji Nelson Chamisa, 45, wa Chama cha Citizens Coalition for Change.

Mjini Harare na jiji la pili kwa ukubwa la Bulawayo, ngome zote za upinzani, vituo vingi vya kupigia kura vilichelewa kufunguliwa wa, na kuwalazimu wapiga kura kusubiri kwa muda mrefu.

Wachambuzi wa mambo walisema, kama ilivyokuwa katika chaguzi zilizopita za Zimbabwe, ZANU-PF, ambayo imekuwa madarakani kwa miaka 43, imekuwa ikitumia taasisi za serikali kuhakikisha itasalia madarakani.

Forum

XS
SM
MD
LG