Tukio hili limetokea Jumatano katika mwezi mtukufu wa Ramadhani kwenye mji mkuu wa Sanaa jioni na kusababisha vifo vya watu 78 na kujeruhi wengine 73, kwa mujibu wa mashahidi na maafisa wa uasi wa kihouthi.
Hili ni janga baya kutokea Yemen kwa miaka mingi ambalo halihusiani na vita vya muda mrefu nchini humo na limetokea siku chache kabla ya sikukuu ya Waislamu ya Eid El Fitri ambayo inaadhimisha mwisho wa mfungo wa Ramadhani baadae wiki hii.
Wanamgambo wa kihouthi walifyatua risasi hewani katika jaribio la kutaka kudhibiti watu wengi na badala yake ilipiga katika nyaya ya umeme na kusababisha kulipuka, hiyo ni kwa mujibu wa mashahidi wawili Abdel Rahman Ahmed na Yahia Mohsen .
Hali hiyo ilisababisha taharuki kwa watu ikiwemo wanawake na watoto kuanza kukanyagana.
Picha za video zilizobandikwa kwenye mitandao ya kijamii zimeonyesha darzeni za miili ya watu wengine wakiwa na hisia kali na wengine wakipiga kelele wakati watu wakijaribu kuwasaidia.
Picha tofauti baada ya tukio zilizotolewa na maafisa wa kihouthi zilionyesha damu, viatu na nguo za waathirika vikiwa vimetawanyika kwenye ardhi. Wachunguzi walionekana katika eneo la tukio kulichunguza eneo hilo.