Wafungwa kadhaa wa kivita wakiwemo raia wa Saudi Arabia waliachiliwa huru Jumamosi kama sehemu ya mabadilishano ya mpakani kati ya ushirika wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia na waasi wa ki-Houthi wanaoungwa mkono na Iran, Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu imesema.
Ndege zinazounganisha Saudi Arabia na eneo linaloshikiliwa na Wa-houthi nchini Yemen ni sehemu ya uhamisho wa siku nyingi uliohusisha karibu wafungwa 900 ambao unakuja wakati kukiwa na mazungumzo ya amani ambayo yameonyesha matumaini ya kumalizika kwa vita vya Yemen vilivyodumu kwa miaka minane.
Ndege ya kwanza ya siku hiyo ilipaa kutoka mji wa kusini mwa Saudi Arabia wa Abha kabla ya saa tatu asubuhi saa za huko ikielekea mji mkuu wa Yemen wa Sanaa unaoshikiliwa na Wa-houthi ikiwa na wafungwa 120 waasi wa ki-Houthi afisa wa masuala ya umma wa ICRC pamoja na mshauri wa masuala ya habari, Jessica Moussan alisema.
Ilifuatiwa na ndege kutoka Sanaa iliyokuwa imewabeba wafungwa 20 wa zamani, miongoni mwao raia 16 wa Saudi Arabia na watatu wa Sudan. Sudan ni sehemu ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia na imetoa wanajeshi wa ardhini kwa ajili ya mapigano hayo.