Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Septemba 22, 2023 Local time: 17:50

Wasomi watatu waunga mkono msimamo wa Wademokrats kumfungulia kesi Rais Trump


Wasomi watatu wa masuala ya katiba na sheria za Marekani wameimarisha kesi ya Wademokrats kwamba Rais Donald Trump amefanya vitendo vinavyostahiki kufunguliwa mashtaka.

Waatalamu hao walikuwa wanatoa maoni yao ya kisheria kuhusiana na uchunguzi uliofanywa na kamati ya upelelezi, unaoonyesha kwamba Rais Trump alitumia vibaya madaraka yake alipoitaka Ukraine kumfanyia uchunguzi mpinzani wake kwa faida zake za kisiasa.

Wademocrats waliitisha kikao hicho cha hadhara wakianza utaratibu wa pili wakisheria wa kutayarisha mashtaka rasmi dhidi ya Rais Donald Trump.

Katika kikao cha Jumatano, kamati ya sheria ilitaka kupata ushuari kutoka kwa wataalamu bingwa wa sheria na katiba kuhusu ripoti ya uchunguzi juu ya kesi ya kumfungulia rais Trump mashtaka mbele ya Baraza la Senate.

Wataalamu wa sheria wakubaliana

Maprofesa watatu kati ya wanne wamesema ushahidi uliokusanywa unadhihirisha wazi Trump alitumia vibaya madaraka yake na inastahiki afunguliwe mashtaka.

Profesa Noah Feldman wa Chuo cha Sheria cha Havard alifafanuwa wazi maana ya kutumia vibaya madaraka.

Aliongeza kuwa utumiaji mbaya wa madaraka hutokea pale rais anatumia sehemu ya mamlaka yake , si kwa maslahi ya Wamarekani bali kwa maslahi yake binafsi, chama chake na maslahi ya uchaguzi.

Wataalamu hao wanakubaliana kwamba utumiaji mbaya wa madaraka ni sehemu ya uhalifu wa hali ya juu katika katiba ya Marekani.

North Carolina

Michael Gerhardt Profesa wa chuo kikuu cha sheria cha North Carolina anasema “ikiwa haya tunayozungumza hapa hayastahiki kumfungulia mashtaka rais, basi hakuna kitu kinafaa cha kumfungulia mashtaka.”

“Hii hasa ndio tabia mbaya ambayo waanzilishi wa taifa waliunda Katiba, ikiwa ni pamoja na kumfunglia mashtaka rais kuilinda nchi”, alisema Gerhardt.

George Washington

Lakini mtaalamu aliyeletwa na wapinzani wa chama cha Republican Jonathan Turley wa Chuo kikuu cha George Washington hakukubaliana na wenzake kikamilifu ingawa alikiri rais alifanya makosa.

Turley alisema ana amini utaratibu huu wa kumfungulia mashtaka rais haujaridhisha na kufikia kiwango cha utaratibu uliyopita na hivyo unabuni tukio la hatari kwa ajili ya utaratibu wa siku za baadae.

Warepublican hawakujali kuwahoji waatalamu hao juu ya masuala ya kisheria lakini waliendelea kuwakosowa wademokrats kwa utaratibu wanaodai unakasoro na uwonevu huku wakimtetea Rais Trump kwamba hajafanya kosa lolote linalostahiki afunguliwe mashtaka.

Mashtaka dhidi ya rais

Hivi sasa kamati ya sheria ya Baraza la Wawakilishi itatayarisha mashtaka rasmi dhidi ya rais, kuhusiana na kadhia hiyo na Ukraine. Hata hivyo kabla ya hapo imepanga kuitisha vikao zaidi wiki ijayo ili kuimarisha hoja yao.

Na hapo tena itafikisha mashtaka hayo mbele ya baraza kamili la wawakilishi ili kupigiwa kura kabla ya mwisho wa mwaka.

Mashtaka yakiidhinishwa yatafikishwa mbele ya baraza la Senate ili kesi kamli ifunguliwa kuweza kumhukumu rais kutokana na mashtaka hayo.

XS
SM
MD
LG