Mwaka huu, anawania nafasi ya urais kwa mara ya tano, baada ya kutofanikiwa katika azma yake ya kuliongoza taifa hilo kwa mara nne, katika chaguzi za awali ambazo, baadhi ziligubikwa na utata.
Katika msururu wa makala yetu maalum kuhusu uchaguzi wa Kenya wa mwaka 2022, leo tunaangazia wasifu wa Raila Amolo Odinga, mwanasiasa mkongwe ambaye, mwaka huu, anawania nafasi ya urais kwa mara ya tano, baada ya kutofanikiwa katika azma yake ya kuliongoza taifa hilo kwa mara nne, katika chaguzi za awali ambazo, baadhi ziligubikwa na utata.
Raila Amolo Odinga, amekuwa katika safu ya siasa za Kenya kwa zaidi ya miongo mitatu, na anakumbukwa zaidi kama kiongozi wa upinzani wa muda mrefu, na ambaye azma yake ya kuiongoza Kenya mara kwa mara imepelekea matukio ya kihistoria yaliyobadilisha taswira ya siasa za nchi hiyo.
Kwenye uchaguzi wa Agosti 9, 2022, itakuwa ni mara ya tano kwa Raila Odinga kuwania urais, na baadhi ya wachambuzi wanasema huenda hii ndiyo nafasi yake bora zaidi ya kupata ushindi, hususan baada ya rais anayeondoka Uhuru Kenyatta, na ambaye kwa kipindi kirefu alikuwa hasimu wake wa kisiasa, kutangaza hadharani kwamba anaunga mgono azma ya Odinga kuwa rais wa tano wa Kenya, na hata kumpigia debe waziwazi. Lakini safari ya kisiasa ya Raila Odinga hadi wakati huu haijawa rahisi.
Mwanawe hayati Mzee Jaramogi Oginga na marehemu Mama Mary Juma, Raila Odinga alizaliwa tarehe 7 Januari 1945, katika mji wa Maseno, wilaya ya Kisumu, nchini Kenya. Baada ya masomo yake aliingia katika utumishi wa umma kwa mara ya kwanza hapo mwaka wa 1974, na kushikilia nyadhifa mbalimbali katika shirika la ubora wa Viwango vya bidhaa la Kenya (KEBS), hadi mwaka wa 1982 alipoanza harakati zake za kisiasa akipinga utawala wa chama cha KANU, ambao ulionekana na wakosoaji kuwa wa kidikteta. Kufuatia jaribio la kuipindua serikali ya Rais Daniel Toroitich Arap Moi, utawala wa Moi ulianza msako kwa lengo la kuwawajibisha waliohusika. Odinga ni kati ya wale waliokamatwa, na baadaye akashtakiwa kwa uhaini na kutumikia vifungo viwili kwa karibu muongo mmoja. Baada ya kuachiliwa katika miaka ya 90, Odinga alikimbia nchi kutafuta hifadhi nchini Norway kwa hofu ya kukamatwa tena na kuteswa zaidi. Martin Oloo ni mchambuzi wa siasa za Kenya.
Alirejea Kenya na kujikita katika harakati za ukombozi kupitia Forum for the Restoration of Democracy (FORD), ambayo wakati huo iliongozwa na miongoni mwa wengine babake, Jaramogi Oginga Odinga na mfungwa mwenzake wa kisiasa Kenneth Matiba.
Aliporudi kutoka uhamishoni, alijiingiza kikamilifu katika siasa, akiungana na babake, makamu wa rais wa zamani, na watetezi wengine kushinikiza serikali ya Moi kufungua nafasi ya kidemokrasia nchini Kenya.
Shinikizo kali zilendelea, kumtaka rais Daniel Arap Moi, kuridhia msukumo wa kubadilisha kipengele cha katiba, kilichoifanya Kenya kuwa nchi ya mfumo wa chama kimoja cha kisiasa. Na hilo lilifanyika mwaka wa 1991.
Kupitia Forum for Restoration of Democracy (FORD), mojawapo ya vyama vya kwanza vya upinzani katika miaka ya 90, Raila alijitoza kwenye
Siasa za kuchaguliwa hapo mwaka wa 1992, alipogomea kiti cha ubunge katika eneo bunge la Langata, nje kidogo ya jiji kuu la Kenya Nairobi.
Baadaye alijitoza kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka wa 1997, bila mafanikio.
Aligombea tena mwaka wa 2007, 2013 na 2017.
Odinga amekuwa mwanachama wa vyama vingi vya kisiasa tangu wakati huo.
Mnamo 2002, alijiunga na vyama vingine vyenye mawazo kama hayo kumfanyia kampeni Mwai Kibaki chini ya Muungano wa National Rainbow Alliance (NARC), muungano ambao hatimaye uliiondoa KANU serikalini na kuleta mapambazuko mapya katika nyanja ya kisiasa ya Kenya.
Kupitia msukumo wa nchi kutaka mabadiliko ya katiba, amekuwa mstari wa mbele, kwanza akiongoza upinzani katika kura ya maoni ya katiba ya mwaka 2005, na kusababisha kutimuliwa kutoka kwa serikali ya Mwai Kibaki, na baadaye kuwa mfuasi wake mkuu mwaka 2010 alipoongoza uungwaji mkono wa kupitishwa kwa katiba.
Lakini wakati historia ya uchaguzi ya Kenya inapoandikwa, ni vigumu kuliacha jina la Raila Odinga nje ya sura ya ghasia mbaya zaidi zilizoikumba nchi hiyo kufuatia uchaguzi mkuu wa mwaka 2007, ambapo yeye na rais wa wakati huo, Mwai Kibaki, walikuwa wakishindania nafasi ya urais. Kilichofuatia ni vurugu, ghasia na umwagikaji wa damu, mabapo inaelezwa kwaba zaidi ya watu 1,200 walipoteza maisha yao, maelgu kujeruhiwa na dazeni za maelfu kufurushwa makwao. Baadaye mirengo miwili ya kisisa, kwa usaidizi wa watatuzi kutoka nje ya nchi, ilikubaliana kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, ambapo Kibaki alikuwa rais huku Odinga akiwa waziri mkuu. Lakini hicho kilikuwa ni kipindi cha miaka mitano tu, kabla hajavalia tena kofia yake ya kiongozi wa upinzani.
Akiwa mkosoaji mkubwa wa serikali katika enzi ya Moi, na baadaye marais Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta, Odinga amekuwa taswira ya siasa za upinzani nchini Kenya kwa kipindi kirefu na aliandika historia kama mwanasiasa wa kwanza aliyefaulu kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais, na kusababisha kufutwa kwa uchaguzi wa kwanza wa urais barani Afrika, hapo mwaka wa 2017.
Baada ya uchaguzi wa marudio wa mwaka 2017, ambao Odinga na wenzake katika muungano wa kisiasa uliopewa jina la NASA walikuwa wameususia, mwanasiasa huyo alipanga hafla ya kujiapisha kama kile alichokiita raisa wa wananchi, na hapo tarehe 30 mwezi Januari mwaka 2018, uapisha huo ukafanyika kwenye bustani za Uhuru Park mjini Nairobi.
Jambo ambalo halikupokelewa vyema na serikali. Kilichofuatia ni n hali ya taharuki, maandamano, uporaji na hata mauaji, huku upinzani na serikali zikiendelea kuchukua misimamo iliyohitilafiana.
Baada ya hapo, Odinga pia aliandika historia kwa kuwa sehemu ya mpango uliofeli wa kutafuta maridhiano ya kitaifa maarufu BBI, kupeana mikono na mpinzani wake wa miaka mingi, Uhuru Kenyatta, hapo tarehe 9 mwezi Machi, mwaka wa 2018, tukio ambalo halikutarajiwa na wengi, na ambalo limeendelea kujadiliwa kwelekea kwa uchaguzi wa mwaka huu.
Odinga amesema mara kwa mara kwamba, iwapo atachaguliwa kama Rais mchakato huo wenye utata, ambao ulisitishwa na mahakama ya juu, kwa kuwa haukufuata mkondo ufaao kwa mujibu wa katiba ya Kenya, utafufuliwa upya.
Tarehe 10 Disema mwaka 2021, Odinga alitangaza kwamba atagombea urais wa Kenya, kauli mbiyu yake ikiwa ni kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini humo.
Chama chake cha ODM kimeshirikiana na vyama vingine, ikiwa ni pamoja na kile kanachotawala hivi sasa cha Jubilee, na kuunda muungano wa upinzani uitwao Azimio la Umoja One Kenya, ambao umeridhia apeperushe bendera yake kama mgombea urais.
Pamoja na kuwa mwanasiasa aliyebobea, Odinga pia ni Mwakilishi Mkuu wa Maendeleo ya Miundombinu katika Tume ya Muungano wa Afrika, nafasi anayoishikilia tangu mwaka 2018.
Iwapo atachaguliwa, Odinga atakuwa Rais aliyeingia madarakani akiwa na umri mkubwa zaidi, katika historia ya nchi hiyo.