Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Machi 04, 2024 Local time: 00:48

Wasifu wa wagombea urais kutoka vyama mbalimbali Kenya


Kampeni ya Jubilee kwenye uwanja wa Homabay magharibi ya Kenya
Kampeni ya Jubilee kwenye uwanja wa Homabay magharibi ya Kenya

Joseph Nyagah

Joseph Nyagah amekuwa kwa siasa za Kenya kwa muda mrefu na ameshawahi kuwa waziri katika serikali ya muungano wa National Alliance Rainbow Coalition (NARC) ulioongozwa na rais Mwai Kibaki. Kabla ya hapo, alikuwa mwandani wa kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), akijiunga na wanasiasa wengine waliounda vuguvugu la “Pentagon.”

Kuelekea uchaguzi wa 2007, Nyagah alitangaza azma yake ya kuwania urais lakini baada ya kufanya makubaliano na wanasiasa wengine wa mrengo wa upinzani, akakubali kumuunga mkono Raila Odinga.

Kwa wakati mmoja, mwanasiasa huyo alikuwa waziri wa ushirika na maendeleo katika serikali ya KANU, wadhifa ambao alijiuzulu kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2002 ili kuwania kiti cha ubunge cha Gachoka katika kaunti ya Embu.

Kabla ya uchaguzi wa mwaka 2013, Nyagah alihama upinzani na kujiunga na muungano wa Jubilee.

Baadaye aliteuliwa mshauri wa masuala ya ushirikiano wa Afrika Mashariki katika serikali ya Uhuru Kenyatta. Alijiuzulu ili kuwania urais akisema kwamba ushauri aliompa Kenyatta kuhusiana na miradi ya miundo msingi ya kuunganisha Kenya na nchi za eneo la maziwa makuu haukutiliwa maanani.

Anatoka kwenye familia iliyobobea kisiasa kwani baba yake, marehemu Jeremiah Nyagah, alikuwa waziri katika serikali zote tatu tangu Kenya kupata uhuru, huku ndugu yake mdogo, Norman Nyagah, akiwa mbunge kwa mihula miwili na pia kiongozi wa walio wengi katika bunge akiwakilisha muungano wa NARC.

Aidha, Joseph Nyagah aliiwakilisha Kenya kama balozi wake nchini Ubelgiji. Kabla ya kutangaza azma yake ya kuwania urais. Nyagah pia alikuwa mhadhiri mkuu wa chuo cha Cooperative University of Kenya , kilicho eneo la Karen, nje ya mji mkuuNairobi. Alizaliwa mwaka wa 1948.

Japheth Kaluyu

Hii ni mara yake ya kwanza kuwania urais. Kaluyu amekuwa akifanya kazi mjini Washington DC kama mshauri wa masuala ya elimu, uwekezaji na afya.

Anaeleza kwenye tovuti yake kwamba ana uzoevu wa utafiti wa kiuchumi na kwamba amefanya kazi kwenyetaasisi za Wall Street mjini New York. Alipata mafunzo yake Marekani na ameshawahi kuhudumu kama mhadhiri wa chuo kikuu. Anasema alizaliwa katika kijiji kidogo katika kaunti ya Kitui.

Kaluyu anasema kwamba anagombea urais kwa sababu, kati ya mengine, angependa kubadilisha maisha ya Wakenya kwa kuongeza nafasi za ajira, hususan kwa vijana na kuchangia kuimarika kwa uchumi na ongezeko la pato la jumla la taifa (GDP) kufikia dola bilioni 150.

Cyrus Jirongo

Cyrus Jirongo amewahi kuwa waziri katika serikali ya KANU iliyoongozwa na rais wa wakati huo, Daniel Arap Moi. Mnamo mwaka 1998, Jirongo alielezea azma yaka ya kuwania urais lakini hii ndiyo mara yake ya kwanza kuwasilisha stakabadhi zake kwa tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na kuidhinishwa rasmi kama mgombea.

Alifahamika sana kama mwenyekiti wa vuguvugu la vijana walikipigia upatu chama cha KANU, katikamiaka ya 90 (Youth for Kanu ’92). Walishirikiana kwa karibu na naibu wa sasa wa rais, William Ruto. Hata hivyo, wawili hao baadaye wakawa mahasimu wakubwa wa kisiasa.

Jirongo anawania uraiskupitia chama cha United Democratic Movement (UDM) na ameeleza kuwa sera zake zitaangazia sana maslahi ya mwananchi wa kawaida. Amewahi kuwa mwenyekiti wa chama cha Kenya African Democratic Development Union (KADDU). Jirongo alizaliwa mwaka wa 1961.

Abduba Dida

Hii itakuwa ni mara ya pili kwa mgombea huyo kuwania urais, baada ya kujaribu bila kufanikiwa kwenye uchaguzi wa 2013. Kitaaluma, Dida ni mwalimu anayetokea eneo la Wajir Magharibi mwa Kenya na kwa muda mrefu amekuwa akijishughulisha na kufanya kazi za kujitolea kuwasaidia watu wa ngazi ya chini katika maeneo mengi ya Kenya.

Kabla ya uchaguzi mkuu wa 2013 nchini Kenya, Dida alielezea kwamba kuwa na mke zaidi ya mmoja kulimsaidia sana katika kupanga kampeni zake kwa uzuri zaidi, akisema mmoja wa wake zake anashughulikia masuala ya kifedha katika familia, mwingine masuala ya kikatibu na mke wa watatu anashughulikia watoto. Alisemahii iliifanya kampeni yake kuwa nyepesi zaidi. Anasimama kwa tiketi ya chama cha Alliance for Real Change.

Dkt Ekuru Aukot

Anafahamika sana kama mmoja wa mawakili waliotayarisha rasimu ya katiba ya Kenya ya mwaka 2010 na anawania uraiskupitia chama cha Thirdway Alliance.

Alikuwa katibu wa kundi lililojulikana kama ‘kamati ya wataalam’ lililokuwa na jukumu la kuweka pamoja maoni ya wakenya kuhusu mabadiliko yaliyohitajika katika katiba ya zamani iliyokuwa ikitumika tangu Kenya kupata uhuru mwaka wa1963.

Ameeleza kwamba ameamua kugombea urais ili kuizuia Kenya “kupasuliwa na ukabila na ufisadi uliokithiri.” Amesema kwamba vuguvugu lake la Thirdway Alliance ambalo liligeuka na kuwa chama cha kisiasa, litaendelea kutumia mitandao ya kijamii kama vile Facebook na Twitter kuhamasisha wa Kenya juu ya umuhimu wa uongozi bora usio na ukabila wala ufisadi. Alizaliwa katika Kaunti ya Turkana katika familia ya watoto 27. Amesema kuwa baba yake alikuwa ameoa wake kadhaa. Ekuru Aukot, ana umri wa miaka 45.

Prof. Michael Wainaina

Dkt. Michael Wainaina alikuwa mhadhiri wa chuo kikuu cha Kenyatta na mchambuzi wa masuala ya siasa ambaye amekuwa akitumia blogu na mitandao ya kijamii kuelezea hisia na ajenda zake.

Anafahamika sana kama mkosoaji asiyeegemea upande wa serikali wala upinzani na anawania kama mgombea huru. Ameeleza kuwa kampeni yake italenga sana masuala ya wanawake na vijana, ambao, anasema, hawashughulikiwi ipasavyo na vyama vikuu nchini.

Ilani yake inaeleza kwamba iwapo atachaguliwa kuwa rais, serikali yake itajenga taasisi ambazo zitakuza taaluma mbali mbali za vijana bali kote nchini.

Anaeleza kwamba kizazi kipya ndicho kinafaa kukabidhiwa uongozi na wapiga kura nchini Kenya.

Wainaina alizaliwa katika kaunti ya Kiambu na ana umri wa miaka 44.

XS
SM
MD
LG