Wakizungumza na Sauti ya Amerika, wachambuzi na wanaharakati wamewataka wanasiasa wanaopinga matokeo ya uchaguzi huo yaliyotangazwa siku ya Jumapili wawakilishe malalamiko yao mahakamani badala ya kuitisha maandamano ambayo yanaweza kuhatarisha maisha ya watu.
Mashariki mwa DRC, watu mbalimbali wamekuwa wakitoa maoni yao kuhusu kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi, ambapo Rais Felix Tshisekedi amepata ushindi mkubwa katika uchaguzi huo, wakati wapinzani wakiendelea kulalamikia zoezi zima la uchaguzi lilivyokwenda.
Mchambuzi na mtafiti wa maswala ya migogoro na usalama Mashariki mwa Congo na Kanda nzima ya Maziwa Makuu Hubert Masomeko amesema ““wapinzani wenyewe wanafahamu walishindwa uchaguzi, ni kweli uchaguzi ulikumbwa na kosoro kadhaa.”
Masomeko ambaye pia anafanyakazi na Shirika la Pole Institut lenye makao yake mjini Goma, Kivu Kaskazini aliongeza
“upinzani unatambua kwamba ulishindwa uchaguzi na Rais Felix Tshisekedi alichaguliwa na raia wa Congo. Nadhani kuliko kuwaita watu kuandamana wakubali matokeo ya uchaguzi, wampongeze Rais Tshisekedi, nwatafute njia ya kuungana naye kwa kulitumikia taifa la DRC.”
Masomeko ameongeza kwamba kinachohitajika sasa ni Rais Felix Tshisekedi kutekeleza ahadi zake kwa raia wa nchi hiyo milioni 100.
“Eneo la mashariki mwa Congo limegubikwa na makundi ya wapiganaji wanaowatesa raia, kama vita vya M23 na miji kadhaa mpaka sasa ikiwa mikononi mwao. Felix Tshesekedi amechaguliwa na wakaazi ahakikishe amani na usalama katika maeneo hayo” alisema Masomeko.
Wananchi wanaoishi Mashariki mwa nchi hiyo wanaomba amani na usalama wakati vita vikiendelea katika sehemu mbalimabli za eneo hilo.
Akitoa maoni yake Josephine Malimukono mkazi wa Goma na kiongozi wa shirika la muungano wa wanawake wa DRC amesema kuwa “matarajio tuliyonayo sisi kina mama kwa Rais tunahitaji kitu kimoja tunayo omba kila siku ni Amani, sababu ni amani inaweza leta maendeleo,”
“katika kampeni yake alisema ataleta amani ,hawa wakimbizi wanao kuwa Mjini Goma na kando kando warudi kwao nyumbani nakuendelea kuishi kama tulivyo kuwa tukiishi zamani” alisema Malimukono.
Akizungumzia ushindi wa Rais Felix Tshesekedi, naye Mwanaharakati wa haki za kiraia Placide Nzilamba alisema
“unaona mwenyewe watu wanasherekea ushindi wa Rais kwani ndiyo changuo lao walikuwa wanasubiri.”
Upinzani ukiwa na siku mbili za kuwakilisha malalamiko yao mahakamani. Usalama umeimarishwa katika maeneo mbalimbali yanayotishiwa na kundi la uasi la M23 pamoja na wapinzani wanaotishia kuandamana.
Mbali na migogoro, wakaazi wa DRC wanaendelea kuusheherekea mwaka mpya katika maeneo ya miji mbalimbali
na baadhi yao wakiwa kambini.
Imetayarishwa na Austere Malivika Sauti ya Amerika, Goma
Forum