Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 02:51

Wananchi wa Algeria waendelea kuuandamana kupinga uteuzi wa rais wa muda


Polisi wawatawanya waandamanaji nchini Algeria.
Polisi wawatawanya waandamanaji nchini Algeria.

Kwa mara ya kwanza katika muda wa wiki saba polisi wa Algeria wamerusha mabomu ya kutoa machozi Jumatano ili kuwatawanya waandamanaji, hasa wanafunzi katika mji mkuu wa Algiers.

Waandamanaji walijitokeza tena Jumatano kufuatia wito wa muungano wa vyama vya wafanyakazi kuandamana ili kupinga kuchaguliwa kwa spika wa baraza dogo la bunge Abdelkader Bensalah kuwa rais wa muda.

Vyama vya upinzani pia vinapinga kuchaguliwa kwa Bensalah, ambaye alikuwa mshauri wa karibu wa rais aliyeondoka madarakani, Abdelaziz Bouteflika, kufuatia kishinikizo la wananchi.

Hapo jana Rais wa muda Bensalah alilihutubia taifa na kuahidi uchaguzi huru na wahaki katika muda wa siku 90 na kuwataka watu kuacha maandamano.

Lakini wanafunzi wakiandamana Jumatano wamekuwa wakipaza sauti zao wakisema “hawajatusikia na tutaendelea kuandamana.”

Wanafunzi, vyama vya kisiasa, pamoja na vyama vya wafanyakazi wanataka kuwepo na kipindi cha mpito kitakachofanya mageuzi makubwa ya utawala na kupanga uchaguzi ulio huru na haki.

Hata hivyo mkuu wa majeshi ya Algeria Luteni Jenerali Ahmed Gaed Salah, amesisitiza kwamba ni lazima katiba ya nchi kuheshimikwa wakati wa mabadiliko haya.

Kulingana na katiba, rais wa nchi akiacha madaraka kwa sababu yeyote ile, ni spika wa baraza dogo la bunge anaechukua madaraka kwa siku 90 wakati ambapo anatayarisha uchaguzi wa rais.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC

XS
SM
MD
LG