Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Mei 28, 2023 Local time: 06:12

Waliobaki Khartoum wahaha maji ya kunywa


Wanaume wakikirejea majumbani mwao wakiwa na chupa za maji wakati mapigano yalipopungua huko Khartoum, tarehe 25 Mei 2023. Picha na AFP.

Mapigano nchini Sudan yamewaacha maelfu ya wakazi wa jiji la Khartoum bila ya maji ya bomba, na huku baadhi yao wakilazimika kuhatarisha maisha yao kwenda kutafuta maji wakati wa kipindi hiki kifupi cha utulivu.

Baada ya karibu wiki sita za mapambano ya mitaani kati ya majeshi yanayowatii majenerali mahasimu huku viwango vya joto vikiwa katika nyuzi joto 40, wakazi wengi wa vitongoji vya kaskazini mwa mji huo mkuu wanahaha wakitafuta maji ya kunywa.

Tarehe 15 Aprili, wakati mapigano yalipozuka kati ya jeshi la Sudan na Kikosi cha Rapid Support Forces (RSF), kituo kinachosambaza maji ya bomba katika wilaya kadhaa za Khartoum Kaskazini kiliharibiwa.

Tangu wakati huo, wakazi wa eneo hilo wapatao 300,000 hawajaona hata tone la maji kutoka kwenye mabomba yao. Baadhi yao wamevifungua tena visima au kutumia masufuria kuchota maji kutoka mto Nile.

"Wakati vita vilipoanza, tulikuwa tukichota maji kutoka katika visima vya viwanda vilivyopo katika eneo la viwanda, lakini wiki moja baadaye, wanamgambo waliliteka eneo hilo," mkazi wa eneo hilo Adel Mohammed aliliambia shirika la habari la AFP.

Mapigano yalilizingira eneo hilo na kufanya vita vipiganwe katika majengo ya hospitali na makazi ya watu, na kumfanya Mohammed kulazimika kusubiri kwa siku kadhaa kabla ya kujitosa nje na kwenda kuchota maji.

Kwa sasa, yeye na majirani zake wanangojea mapigano yapungue kwa muda ili wachukue masufuria, beseni na majagi kuelekea kwenye kingo za Mto Nile, ambao unapita katika vitongoji vya jiji la Khartoum.

Kwa pamoja, wanajaza gari na kurudi kusambaza lita chache za maji kwa kila familia zilizobaki katika katika kitongoji hicho.

Lakini wengi wao wameondoka.

Forum

XS
SM
MD
LG