Hii inatokea wakati wahamiaji zaidi wakianza kukata tamaa ya kuingia kiusalama ndani ya Umoja wa Ulaya.
Serikali ya Kurdistan na maafisa kwenye uwanja wa ndege wa Erbil wamesema ndege hizo zimewasili mapema Jumatano katika mji wa jimbo la Erbil lenye utawala wa ndani la Wakurdi, zikibeba Wairaqi 600, wengi wao wakiwa Wakurdi.
Abiria wengi wamesema wamepata afueni kurudi nyumbani.
Malak Hassan mwenye umri wa miaka 11 ambaye familia yake ilijaribu kuvuka mpaka wa Belarus na kuingia ndani ya Umoja wa Ulaya amesema, “sitaki kurudi kwenye njia hiyo, ilikuwa mbaya, kulikuwa mvua nyingi na theluji”.
Naye Awat Qader kutoka Kurdistan amesema aliona wahamiaji wakipigwa wakati wakipiga kambi karibu ya mpaka wa Belarus na Lithuania, na kwamba hatajaribu kufanya safari hiyo tena.
Wairaqi ambao walikimbia nchi yao ili kutafuta fursa za kiuchumi na wengine wakitafuta hifadhi ya kisiasa, walianza kurejea nchini mwao wiki moja iliyopita, baada ya kushindwa kuingia Umoja wa ulaya kupitia njia ambayo wasafirishaji haramu waliahidi itawasadia kufika wanaokwenda.
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la Reuters