Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Desemba 06, 2024 Local time: 12:03

Tanzania: Kikosi Kazi Kupambana na Uzalishaji wa Pombe ya 'Viroba'


Waziri January Makamba
Waziri January Makamba

Tanzania imepiga marufuku kuuza pombe zilizo katika mifuko ya plastiki maarufu kama "viroba".

Akizungumza na vyombo vya habari Dar es Salaam, Tanzania Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema ifikapo Machi 1, viroba havitaruhusiwa kutumika na itakuwa ni kinyume cha sheria kwa yoyote atakayefanya hivyo.

Katika kusisitiza hilo Jumatatu Serikali ya Tanzania, kupitia Waziri wake wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), January Makamba ametangaza kuwa tayari kuna kikosi kazi cha taifa cha kufuatilia pombe kali zinazofungwa kwenye pakiti za plastiki maarufu kama “viroba.”

Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ameongea Jumatatu na waziri Makamba kuhusu suala hili ambalo kwa mara ya kwanza lilitangazwa na waziri mkuu.

Makambaametoa ufafanuzi kuhusu madai ya kwamba kwa nini tangazo hili limekuja ghafla na muda uliotolewa na serikali ulikuwa mdogo sana.

Amesema sheria za Tanzania, zinaeleza kwamba umri wa mtu kuweza kunya pombe ni miaka 18.

“Lakini pamoja na kuwepo hiyo sheria watoto wadogo tayari wameonekana kuwa ni wenye kuathirika na utumiaji viroba kutokana na urahisi wa upatikanaji wake,” amesema waziri huyo.

Waziri Makamba amesema kuwa mwaka jana serikali ya Tanzania iliteketeza tani 3 ya viroba feki wilayani rombo mkoani Kilimanjaro.

Pia Naibu Waziri wa Afya wa Tanzania Hamisi Kiganwala alikifungia kiwanda cha Afro – America kilichokuwa kinazalisha viroba feki. Tafiti nyingi zinaonyesha matukio ni mengi lakini kwa uchache hali ni hiyo hivi sasa Tanzania na matukio mengine yanajumuisha vifo.

Wakati huo huo Kamanda wa polisi wa kikosi cha barabarani nchini Tanzania, Mohamed Mpinga, ameeleza kwamba amri hiyo itasaidia kupunguza ajali za barabarani kwa sababu matumizi makubwa ya pombe hiyo yapo kwa vijana wakiwemo madereva wa bodaboda, daladala ama matatu na makondakta.

Hali kadhalika mamlaka ya chakula na dawa nchini Tanzania ilishawahi kutangaza hatari ya matumizi ya pombe hiyo ya viroba kuwa ni hatari kwa maisha ya wanywaji kutokana na ugumu wa kugundua uhalali wa pombe hizo.

Kwa mfano kikosi maalumu cha mamlaka ya mapato Tanzania TRA mkoani Kagera nchini Tanzania, kilishawahi kunasa shehena ya pombe kali aina ya viroba yenye thamani ya shilingi miliono 200 zilizokuwa zikiingizwa nchini Tanzania kinyume cha sheria.

Ikumbukwe kwamba kiroba si jina la pombe bali ni mifuko ya plasiti ambayo inatumika kufungia pombe kali. Nchini Tanzania pombe ambazo zimekuwa zikitumia mfumo huo, inajumuisha pombe maarufu ya Konyagi, lakini pombe nyingine ni Zed,Raider, Empire, na Signature, na pombe nyingine ambayo yenyewe imepewa jina hilo la mifuko ya plasiti ya Kiroba.

Pombe hizo zimekuwa zikiuzwa kati ya shilingi 300 mpaka 500 za kitanzania. Kwa mfano kwa uchunguzi uliofanywa na gazeti moja nchini Tanzania limeonyesha kwamba tofauti na matarajio ya wazazi na walezi wengi idadi kubwa ya wanafunzi waliopo mijini hasa wa shule za sekondari hutoroka na kwenda kunywa viroba.

Katika utafiti huo uliofanyika katika shule za msingi na sekondari katika manispaa ya Ilala, Temeke na Kinondoni jijini Dar es salaam nchini Tanzania, inaonyesha kuwa utumiaji wa pombe ni wa kawaida kuliko ilivyodhaniwa. Lakini licha ya hayo wanyaji hawakosi la kusema.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Iddi Ligongo, Washington, DC

XS
SM
MD
LG