Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Februari 08, 2023 Local time: 11:09

Utulivu warudi Tripoli baada ya kuondoka kwa waziri mkuu wa serikali ya upinzani Libya


Waziri mkuu wa mpito wa Libya Abdulhamid Dbeibah atembelea mtaa wa Tripoli ulokumbwa na vita Jumanne

Waziri mkuu wa mpito wa Libya, Abdulhamid Dbeibah amekutana na wakazi wa mtaa wa mji mkuu wa Tripoli, uloshuhudia mapigano makali alfajiri ya Jumanne.

Mapigano yalizuka baada ya wapiganaji wa serikali ya upinzani yenye makazi yake mjini Tobruk, kujaribu kuingia kwa nguvu mashariki mwa mji huo, wakifuatana na waziri mkuu aliyeteuliwa na bunge, Fathi Bashagha, pamoja na baadhi ya mawaziri wake.

Ofisi yake ilitangza baadae kwamba Bashagha anaeungwa mkono na Khalifa Haftar, kiongozi wa kijeshi aliyeasi wa eneo la mashariki, aliondoka Tripoli asubuhi ya Jumanne kwa ajili ya usalama wa wananchi.

Haijafahamika bado ikiwa kuna majeruhi kutokana na mapigano hayo ambayo yanaweza kutishia usalama ulopatikana Libya kwa miaka miwili sasa na kutumbukiza nchi hiyo kwenye vita virefu.

Umoja wa mataifa na Umoja wa Ulaya zimetoa taarifa kutaka utulivu udumishwe na kuwataka wanasiasa wa Libya kuelewana.

Mvutano wa kisiasa umesababisha kukwama kwa kazi za serikali na hasa kufungwa kwa sehemu viwanda vya kuzalisha mafuta, na hivyo kupunguza kwa karibu nusu mapato ya kigeni ya nchi hiyo.

Juhudi za kidplomasia kujaribu kutanzua mzozo huo wa kisiasa zina kwenda pole pole, na wachambuzi wanasema tukio la Jumanne linaweza kuathiri sana juhudi hizo.

Mkuu wa masuala ya kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell amesema kwamba hali inazidi kua mbaya zaidi.

“Tulitarajia kitu kama hicho kutokea, kwa sababu,” anasema “nchini Libya uchaguzi haujafanyika na kuna serikali mbili zinazopingana.”

Ubalozi wa Marekani umezihimiza pande zote mbili kujizuia kutumia ghasia na kwa viongozi wa kisaisa kutambua kwamba kunyakua madaraka kwa nguvu kutaumiza tu wananchi wa Libya.

Kumekuwepo na serikali mbili zinazokinzana Libya tangu mwezi Februari mwaka jana, baada ya wanasiasa kushindwa kukubaliana na mpango wa kuitisha uchaguzi wa rais na bunge na muda wa mhula wa Waziri mkuu Dbeibah kumalizika, na kukata kuondoka madarakani.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG