Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Julai 22, 2024 Local time: 20:20

Trump atetea amri ya kuwazuia wahamiaji


Maandamano yakupinga amri ya kiutendaji ya Rais trump kuzuia wahamiaji.
Maandamano yakupinga amri ya kiutendaji ya Rais trump kuzuia wahamiaji.

Rais wa Marekani, Donald Trump ameendelea kuitetea amri yake ya kiutendaji inayozuia kuingia nchini wakimbizi na watu kutoka nchi saba zenye waislamu wengi.

Makundi yanayotetea haki yameapa kuendelea kushinikiza hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya amri hiyo, na maelfu ya watu wamekuwa wakipinga amri hiyo katika miji ya kote nchini Marekani ikiwa pia wademokrat wamejiandaa kuanzisha sheria itakayozuia amri hiyo.

Katika mlolongo wa ujumbe mfupi wa Twitter Jumatatu asubuhi, Trump amesema Waziri wa Usalama wa Ndani, John Kelly amemueleza “kila kitu kinaenda vizuri na yapo matatizo machache .”

Ameongeza kuwa “matatizo makubwa katika viwanja vya ndege” yamesababishwa na kuharibika kwa kompyuta kuliko kukwamisha shughuli za shirika la ndege la Delta, waandamanaji, “na machozi” ya kiongozi wa walio wachache katika Seneti, Chuck Schumer.

Schumer alionekana Jumapili akijizuia kutoa machozi wakati akimwambia Trump kuondoa amri ya kiutendaji.

Amri hiyo iliyosainiwa Ijumaa imesitisha kwa siku 120 wakimbizi kuingia nchini na hivyo hivyo kukataza kwa siku 90 wananchi kutoka Iraq, Iran, Syria, Somali, Sudan, Libya na Yemen.

Amri yawachanganya wengi

Hata hivyo utekelezaji wake umewachanganya wengi, hasa katika viwanja vya ndege vya taifa, ambapo baadhi ya watu wenye hatia ya ukazi halali yaani "green cards" kama walishikiliwa kwa ajili ya mahojiano ya ziada kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini.

Waziri wa Usalama wa Ndani Kelly ametoa tamko Jumapili akifafanua kuhusu sera hiyo, na kusema anazingatia kuwa “kuingia kwa wakazi wakudumu halali nchini ni kwa maslahi ya taifa.”

Katika tamko jingine, Idara ya mambo ya ndani imesema serikali inahaki ya kufuta viza yeyote wakati wowote pale inapoona ni muhimu kwa usalama wa taifa.

Hilo lilifuatiwa na amri ya dharura ya muda iliyotolewa na mahakama kuu huko New York ikikataza kuondoshwa nchini kwa watu wenye kuwasili katika viwanja vya ndege wakiwa na viza halali au kibali cha kuingia nchini kama mkimbizi.

Jaji Ann Donnelly ameandika, “ Kuna hatari ya wazi kuwa, iwapo hakutakuwa na amri ya kuwawezesha kubakia nchini, kutakuwa na maumivu yasiyokadirika kwa wakimbizi, wenye viza na watu wengine kutoka mataifa mengine” ambao wanazuiliwa na amri ya rais.

Trump amerejea kutaka usaili wa kina ufanyike kwa wakimbizi, na maafisa wa ngazi ya juu wa serikali waliokuwa wakiongea na waandishi Jumapili wameelezea kuwa mfumo wa zamani ulikuwa ni “mbovu mno.”

Chini ya Uongozi wa Obama.

Chini ya uongozi wa rais Barack Obama wakimbizi walitakiwa wapitie katika uhakiki wa kiusalama, ikiwemo kutathminiwa na maafisa wa polisi na vyombo vya kipelelezi na usaili wa kina kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini. Kwa wakimbizi wengi, mchakato huo ulikuwa unachukuwa hadi miaka miwili.

Rais Barack Obama
Rais Barack ObamaNihad Awad, mkurugenzi mtendaji wa Baraza la Mahusiano kati ya Marekani na Uislamu, ameiambia VOA kuwa amri ya Trump inakwenda kinyume na maadili ya wamarekani ambayo historia inaonyesha kuwa wamekuwa wakiwakaribisha wale wanaokimbia vita na mateso.

“Donald Trump hajaweza kumshawishi yeyote kati yetu kwamba ana wasiwasi wa msingi ulioegemea sheria au usalama wa taifa.

Kwa mfano, wakimbizi wa Syria tayari wanapitia uchunguzi usiopungua miaka miwili na kutathminiwa kwa kina na pindi wanapowasili nchini hakuna wasiwasi juu yao kwani wamechunguzwa.

Hakuna Shambulizi la Kigaidi

Hakuna shambulizi la kigaidi ambalo limehusisha mkimbizi wa Syria au mkimbizi mwengine ambaye tunamjua,” Awad amesema. “Kwa hiyo Trump kuegemea amri ya kiutendaji katika dhana potofu sio umarekani, na kinyume cha maadili".

Nchi 57 za Umoja wa Ushirikiano wa Mataifa ya Kiislamu (OIC) umesema Jumatatu kuwa hatua aliyochukuwa Trump inaendelea kusababisha ugumu katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili wakimbizi.

“Kitendo cha kuzichagua na kuzibagua nchi hizi itapelekea kuendeleza kauli kali za watu wenye misimamo mikali na itawapa nguvu watetezi wa uvunjifu wa amani na ugaidi katika wakati huu mgumu ambapo OIC imekuwa ikifanya mazungumzo na washirika wake wote, ikiwemo Marekani, katika juhudi za kupambana na misimamo mikali na ugaidi katika namna zake zote na udhihirisho wake,” imesema taarifa ya OIC.
Nchi zote saba zilizoorodheshwa katika amri ya kiutendaji ni wanachama wa OIC.
Nakala ya amri inazungumzia shambulizi la kigaidi la Septemba 11, 2001 lililouwa takriban watu 3000 Marekani, lakini haiihusishi Saudi Arabia, ambapo wengi kati ya watekaji wa ndege walitokea huko.

Historia ya ugaidi

Iran, Syria na Sudan wako katika orodha ya Wizara ya Mambo ya Nje ikiwaelezea kama wadhamini wa ugaidi, wakati Iraq, Libya, Yemen na Somalia zimeorodheshwa kama ni maficho ya magaidi.

wapiganaji wa al-Qeida
wapiganaji wa al-QeidaWaziri wa Habari wa Sudan Ahmed Bilal ameiambia i VOA kuwa nchi yake ina matumaini kuwa Trump ataondoa amri hiyo baada ya siku 90.Anasema anafikiria kuwa amri hiyo itaiharibia Marekani kwa kujitenga na ulimwengu.”

Pia amesema kuwa Sudan ilikuwa ina matumaini ya kuboresha mahusiano yake na Marekani, na hakuna sababu kwa Sudan kuwa katika orodha ya wale wanaodhamini ugaidi.

Tuhuma hizo zimekuwepo tangu mwaka 1993 juu ya wasiwasi kuwa Sudan inasaidia vikundi vya kigaidi kama vile Hamas na Hezbollah, na nafasi yake katikati ya miaka ya 90 kuwa ni maficho na eneo la kuwapa mafunzo vikundi kama vile al-Qaida.

Maseneta wa muda mrefu wa Marekani, John McCain na Lindsey Graham, ambao pia ni wajumbe wa Kamati ya Seneti ya Huduma za Kijeshi wameikosoa amri ya Trump Jumapili, wakisema mkanganyiko uliotokea katika viwanja vya ndege inaonyesha hatua zilizochukuliwa hazikufanyiwa tathmini vizuri.

“Tuna wasiwasi hasa na ripoti kuwa hii amri ilianza kutekelezwa pengine bila ushauri au kwa ushauri mdogo sana na wizara ya Mambo ya Nje, Ulinzi, Sheria na Usalama wa Ndani,” walieleza katika taarifa yao ya pamoja. “Mchakato huu wa haraka haraka una hatari ya kuleta madhara.”.

Trump amejibu kwa Twitter, akimwita McCain na Graham “ dhaifu katika masuala ya wahamiaji” wakisema wao wanatakiwa walitupie macho suala la Islamic State, uhamiaji haramu na usalama wa mipaka.

Wasemavyo maseneta
Seneta Chris Murphy, mdemokrat ameyaita maneno ya McCain na Graham ni “yenye nguvu” na kuwataka wafanye kazi pamoja katika suala hilo.

Seneta Lindsey Graham(L) na Seneta John McCain
Seneta Lindsey Graham(L) na Seneta John McCain

“Nitapeleka mswada wiki ijayo ili kuiondoa amri hii hatari, na ya chuki,” alioposti kwenye twitter.

Kiongozi wa waliowengi katika Seneti, Mitch McConnell amesema anaafiki Jumapili kuzidishwa kwa uchunguzi wa kina, lakini hakubaliani na vigezo vya kidini.

“Nafikiri ni fikra nzuri kuwa na mchakato madhubuti wa tathmini hizi,” ameliambia shirika la ABC News.

Seneta wa Republikan Jeff Flake wa Arizona amesema Trump yuko sahihi kuwa na wasiwasi juu ya usalama wa taifa, “lakini haikubaliki ikiwa hata watu wenye hati za ukazi halali wa kudumu wanatiwa ndani au kurejeshwa.

Wasafiri wapata usumbufu mkubwa

Raia wa Iran Neda Daemi, mwenye umri wa miaka 28, ambaye amekuwa mkazi wa kudumu Marekani kwa miaka 16 aliruhusiwa baada ya kushikiliwa kwa saa 10 Jumamosi. Daemi amezungumza na mawakili wawili na amesema hakutakiwa kusaini makaratasi yeyote. Anasema alisafiri kwa ndege mpaka Los Angeles akitokea Tehran ambako alikuwa akiitembelea familia yake.

Mkimbizi wa Kisomali Binto Siyad Aden na watoto wake waliachiwa baadae Jumamosi jioni baada ya kuzuiliwa huko Virginia. Walikuwa wanarejea kupitia viza ya kuunganisha familia kutoka Kenya.

Mumewe Aden, Farhan Suluh Anshur- Mmarekani kutoka Minnesota- amesema anaamini mkewe na watoto wake wawili waliachiwa baada ya mahakama kuingilia kati.

“Huwezi ukawa na picha ya furaha yetu na hisia zetu sasa. Wameachiwa na sasa hivi tuko pamoja katika hoteli karibu na uwanja wa ndege,” Anshur amesema.

Amewaambia waandishi kuwa mkewe alinyanyaswa na maaskari wakati akiwa ameshikiliwa hapo uwanja wa ndege.

“Walimsumbua na kumtishia kwa kumfunga pingu na kumweka chini ya ulinzi; walimlazimisha kusaini fomu inayosema kwamba yeye na watoto wake wataondolewa nchini, lakini akakataa kusaini kwa ajili ya watoto wake akiwaambia baba yao ni raia wa Marekani,” amesema.

XS
SM
MD
LG