Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 29, 2022 Local time: 07:02

Uganda yapata soko la sukari Tanzania


Rais Museveni na Rais Magufuli

Serikali ya Tanzania imefanya makubaliano ya kuanzisha ununuzi wa sukari kutoka nchini Uganda, badala ya kuagiza kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kunapokuwa na upungufu wa bidhaa hiyo.

Hatua ya Tanzania, inajiri mwaka mmoja baada ya wanasiasa wa Kenya kukataa uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka Uganda kwa msingi ya kuwa itaua viwanda vyake.

Hivi sasa ni mwaka mmoja tangu siasa za sukari kutishia uhusiano kati ya Kenya na Uganda.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari nchini Uganda, Tanzania imefungua soko lake kwa Uganda, na imeruhusu kuingiza bidhaa bila kizuizi chochote.

Rais John Magufuli na mwenzake Yoweri Museveni wa Uganda, wamekubaliana kuwa wafanyabiashara wa sukari kutoka Tanzania, watakuwa wakiagiza bidhaa hiyo kutoka Uganda, badala ya kuagiza kutoka Brazil na Thailand.

Wakati huo huo Waziri wa Biashara na Viwanda Uganda Amelia Kyambadde amefafanua kuwa ushirikiano wa aina hii ndio unaotakikana baina ya nchi hizi za Jumuiya.

"Ni vyema kama makubaliano yaliyopo kwenye mkataba yataheshimika ili kwamba kama mwenzako ametengeneza bidhaa za ziada, jambo lililo bora ni kununua kutoka kwake kuliko kutafuta bidhaa hiyo nje ya muungano," amesema.

Magufuli, ambaye amewasili nchini Uganda siku chache kabla ya mkutano wa 19 wa marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao unatarajiwa kuanza baadaye wiki hii, amefanya mazungumzo ya kuimarisha biashara kati ya nchi hizo mbili, miezi miwili baada ya viongozi hao kukubaliana kujenga bomba la mafuta kutoka mjini Hoima nchini Uganda hadi Tanga, Tanzania.

Naye Museveni ameeleza kwamba Uganda inatengeneza kiasi kikubwa cha sukari, tani 125,000 ambazo hadi hivi sasa hazipati wanunuzi. Tanzania kwa upande wake ina uhaba wa tani 100,000 za sukari kila mwaka.

Mnamo mwaka 2016, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alifanya makubaliano na Rais Yoweri Museveni kuruhusu Uganda kuuza sukari nchini Kenya, makubaliano yaliokosolewa sana na wanasiasa nchini Kenya na hatimaye kuzuiwa.

Hata hivyo Kenya inaagiza sukari kutoka Brazil, ikidai kwamba Uganda nayo huagiza sukari kutoka Brazil, na kuiweka katika mifuko upya ya viwanda vya Uganda na kuuza katika nchi wanachama kwa bei rahisi.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennes Bwire, Washington DC

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG