Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Februari 07, 2023 Local time: 13:40

Tshisekedi ameapa kujenga jeshi lenye nguvu na 'kukomesha madharau kutoka kwa majirani'


Rais wa DRC Felix Tshisekedi akiwa na makamanda wa jeshi la nchi hiyo, July 11, 2020

Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi amesema kwamba atafanya kila awezalo kuhakikisha kwamba jeshi la nchi hiyo lina nguvu na uwezo wa kulinda nchi dhidi ya kila aina ya adui.

Tshisekedi amesema kwamba Congo imekuwa ikivamiwa na makundi ya waasi pamoja na wanajeshi kutoka nchi Jirani kwa sababu jeshi lake limekosa ujuzi, uwezo na mwongozo dhabithi kwa muda mrefu.

Ameapa kuhakikisha kwamba jeshi la FARDC linapokea mafunzo ya kisasa na linarudusha heshima yake.

Alikuwa akihutubia wanajeshi waliopokea mafunzo, katika kambi ya jeshi ya Kitona, katikati mwa Congo, aliposema kwamba “maadui wa DRC wamedharau na kuichezea Congo kwa sababu jeshi lake limekosa usimamizi mwafaka kwa muda mrefu.”

“wamefanya kila wawezalo kudhoofisha jeshi wanajeshi wetu. Sitaruhusu hilo kuendelea kufanyika.” Amesema Tshisekedi alipotembelea wanajeshi waliosajiliwa hivi karibuni na wanaopokea mafunzo, na kuwahakikishia kwamba serikali yake itatoa msaada unaohitajika kuhakikisha kwamba wanafanikiwa katika kazi yao.

Majibizano kati ya DRC na Rwanda

Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo imeshutumiana na Rwanda katika siku za hivi karibuni, kila upande ukidai kuunga waasi wenye lengo la kutatiza usalama kila upande.

DRC inadai kwamba Rwanda inaunga mkono waasi wa M23 wanaopigana na wanajeshi wa serikali mashariki mwa DRC.

Rwanda inadai kwamba DRC inaunga mkono waasi wa FDLR wenye lengo la kutatiza usalama wa Rwanda.

Mapema mwezi huu, rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi alidai kwamba utawala wa Rwanda, unaoongozwa na rais Paul Kagame, “ni adui wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo,” na kwamba “raia wa Rwanda ni ndugu wa Congo, wanaostahili kusaidiwa kuwa huru.”

Kati ya wanajeshi wanaopokea mafunzo, 300 ni wanawake.

Tshisekedi ameahidi kutatua changamoto wanazokumbana nazo, pamoja na familia zao.

“Shida zenu sasa ni shida zangu,” ametangaza Tshisekedi akiongezea kwamba “tuwe na nidhamu katika kila mnalofanya ili kuwalinda raia ambao ni ndugu na dada zenu ambao wamedhulumiwa kwa muda mrefu.”

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG