Ziara za viongozi zilizofululiza mjini Washington zimetafsiriwa na wengi kama ni juhudi za viongozi hao za pamoja kumshawishi Rais Trump kutotupilia mbali makubaliano ya nyuklia ya Iran na kuondoa ushuru wa kudumu kwa vyuma na aluminium kwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.
Wakati mshikamano wa Trump na Macron uliojulikana kama “bromance” ukijieleza waziwazi wakati Macron alipotembelea Marekani, mahusiano ya Trump na Merkel bila ya shaka yanajulikana kuwa ya kawaida. Imeripotiwa kuwa wakati wa mkutano wao mwezi Machi 2017, Trump alionekana kujizuia kupeana mkono na Merkel, na viongozi hao hawakuzungumza kwa miezi mitano mpaka walipowasiliana Machi 1, kwa njia ya simu.
"Wakati Emmanuel Macron ni mwenye mafanikio zaidi katika kumuonyesha bashasha Rais Trump wakati wanapokutana, Angela Merkel hatumii bashasha kama ni kipaumbele chake katika mazungumzo, na badala yake husimamia misingi, maadili ya pamoja na maslahi ya pande zote," amesema Erik Jones, mkurugenzi wa Idara ya Tafiti za European na Eurasian katika chuo kikuu cha Johns Hopkins.