“Tunaamini kuwa lazima hatua fulani zichukuliwe nchini Kenya na pia yawepo marekebisho ya hatua zilizochukuliwa, kama vile kufunga vituo vya televisheni na kutishia uhuru wa mahakama,” amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson.
"Nafahamu kuwa Kenya inatizama masuala haya kwa umakini wa hali ya juu. Vyombo vya habari huru na binafsi ni muhimu katika kulinda demokrasia na kuwapa wananchi wa Kenya imani na serikali yao,” ameongeza.
Serikali ya Kenya ilivifungia vituo vitatu vya televisheni mwezi Januari 2018, siku ambayo Odinga alijiapisha mwenyewe katika sherehe za kuigiza kuapishwa rais. Serikali ilikiuka amri ya mahakama iliyokuwa inataka vituo hivyo vifunguliwe, ambavyo vilipanga kuonyesha kujiapisha kwa Odinga.
Wakati huohuo Waziri Tillerson ameshindwa kuhudhuria shughuli alizokuwa amepangiwa kuzifanya Jumamosi katika siku ya pili ya ziara yake nchini Kenya "kwa kuwa hajisikii vizuri", msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amesema.
"Baadhi ya matukio muhimu aliyokuwa ahudhurie yatafanyika bila ya yeye kuwepo, na wanaangalia uwezekano wa kubadilisha wakati wa matukio mengine," amesema Goldstein, naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani.
Tillerson , miaka 65, yuko katika siku ya nne ya ziara yake ya kwanza ya kidiplomasia katika bara la Afrika, ambako tayari ametembelea Ethiopia, Djibouti na Kenya na amepangiwa kwenda Nigeria na Chad.