Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Aprili 24, 2024 Local time: 10:04

Tanzania yafafanua visima vya urefu gani vinahitaji vibali


Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo
Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo

Serikali ya Tanzania imetoa ufafanuzi juu ya visima vilivyo chimbwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida kuwa havihitaji kibali.

Kwa mujibu wa gazeti la Mtanzania serikali imeeleza kuwa mtu yeyote ambaye amechimba ama anatarajia kuchimba kisima kinachozidi matumizi ya kawaida, yaani zaidi ya mita 15, anapaswa afuate taratibu za kuchukua kibali.

Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji namba 11 ya mwaka 2009 kifungu cha 43(1) ambacho kinamtaka mtu yeyote anayetaka kuchepusha, kukinga, kuhifadhi, kuchukua na kutumia maji kwenye chanzo cha maji juu ya ardhi au kujenga miundombinu yeyote kuomba kibali.

Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema hadi sasa kuna maeneo 23 tu ambayo yana shida ya maji na tayari yameshawekewa matanki kwa ajili ya kusaidia uvunaji na usambazaji wa maji.

“Kwa watu wanaochimba visima vya maji kwa ajili ya matumizi ya kawaida hahitaji kibali, lakini wale wanaotumia visima ambavyo vipo zaidi ya mita 15, lazima wafuate taratibu ikiwemo kulipia huduma hiyo,” alisema Profesa Mkumbo.

Aliwaambia waandishi wa habari Serikali imeweka utaratibu huo muda mrefu isipokuwa umeanza kutiliwa mkazo kwa sasa kutokana na hali ya upatikanaji wa huduma za maji kuwa nzuri.

Alisema lengo si kuwakomoa wananchi bali ni kumfanya mtu kutumia maji bila kuathiri watu wengine.

Kwa upande wake Makonda alisema hali ya upatikanaji wa maji kwa Jiji la Dar es Salaam kwa sasa ni nzuri na kwamba katika maeneo mablimbali ikiwemo Ilala na Kigamboni asilimia 40 ya wakazi wake hawana maji.

Profesa Mkumbo aliwataka Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (Dawasa), kuhakiki na kutambua visima vilivyopo ili viweze kufuata taratibu hizo.

Katika hatua nyingine, Profesa Mkumbo, amesema Serikali imeanza kujiandaa kuvuna maji ya bahari ili yaweze kutumika katika Jiji la Dar es Salaam baada ya mwaka 2035.

“Mwaka 2030 Jiji la Dar es Salaam linakadiriwa litakuwa na watu milioni kumi, hivyo mahitaji ya maji yatakuwa makubwa, ili kukidhi mahitaji hayo Serikali imejipanga kuvuna maji ya bahari ambayo yatakuwa yanatumika katika jiji hilo lengo ni kuhakikisha tunaondoa adha ya maji,” alisema Profesa Mkumbo.

XS
SM
MD
LG