Watoto nao wameitaka serikali yao kuwapeleka elimu huko vijijini ambako wazazi na walezi wamekuwa wakiwaruhusu watoto wao kwenda mjini kutafuta kazi na hivyo kulazimika kukatiza masomo.
Suala ambalo limeungwa mkono na wanasheria ambapo wamesema kuweka sheria bila ya kuwapa elimu wananchi haitakuwa na matokeo mazuri katika kumaliza vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.
Watoto bado wanakabiliwa na changamoto ya vitendo mbali mbali vya ukatili ikiwa ni pamoja na ubakaji, ulawiti, ukeketaji, ndoa za mapema na mimba za utotoni.
Kwa mujibu wa taarifa za jeshi la Polisi, mwaka 2022 kulikuwa na jumla ya matukio 12,163 yaliyoripotiwa ukilinganisha na matukio 11,499 kwa mwaka 2021 sawa na ongezeko la matukio 664 (asilimia 5.8).
Takwimu hizo zimeonyesha kuwa matukio hayo yanawaathiri zaidi watoto wa kike kuliko wa kiume, Shilo Kosimasi ni miongoni mwa watoto wanaolelewa katika kituo cha Kiwohede kilichopo Bunju jijini Dar es Salaam amesema ili kutokomeza vitendo vya ukatili serikali iende kutoa elimu vijijini kwa vile watoto wengi wa mitaani wamekuwa wakitokea huko mara wanapomaliza elimu ya msingi.
‘‘Watoto wa mitaani huku Dar es Salaam ni wengi ambao wanaotokea mikoani kwahiyo naishauri serikali ipeleke elimu vijijini kwa wazazi haswa na waonywe watoto wanapo maliza elimu ya msingi wasiachwe kuzurura mitaani na wengine kufanya kazi za ndani na wazazi wanaona ni jambo la kawaida, kwa sababu watoto wanaleta kipato nyumbani,’’ ameongezea Kosimasi
Aidha ripoti ya Hali ya Ukatili wa Watoto Mtandaoni ya mwaka 2022 inaonyesha nchini Tanzania asilimia 67 ya watoto wenye umri kati ya miaka 12 – 17 hutumia mitandao ikiwemo simu na intaneti. Taarifa hiyo pia inaeleza kuwa asilimia 4 ya watoto ni wathirika wa aina mojawapo ya ukatili wa mtandaoni ikiwemo kulazimishwa kujihusisha na vitendo vya kingono, kusambazwa picha na video zenye maudhui ya kingono bila ridhaa yao.
Suala ambalo watetezi wa haki za binadamu wanawataka wazazi na walezi kusimamia vizuri matumizi ya kidijitali ili kuwasaidia watoto kujifunza kupitia elimu pamoja na kuongeza ubunifu kupitia mitandao hiyo.
Vaillet Mollel Mkurugenzi Msaidizi katika mradi wa kizazi hodari kanda ya Kaskazini Mashariki amesema,
‘‘Wazazi vijijini wakati mwingi wanakuwa katika shughuli za uzalishaji kwa mfano migodini, mashambani, au kwenye shughuli za ufugaji kwahiyo wanakuwa hawana muda wa kuwafuatilia watoto wao kwahiyo wanapo kutana na watoto wengine kutoka mijini inakuwa rahisi kujifunza na kuona kumbe mjini ni sehemu nzuri’’
Tanzania bado inakabiliwa na tatizo la kuwafanyisha kazi watoto huku pakiwa na baadhi ya maeneo kutotolewa taarifa za moja kwa moja na wengine wakiwa hawajui mahali pakwenda kutoa taarifa hizo wanasheria wanasema katika masoko ni miongoni mwa sehemu ambazo watoto wanatumikishwa katika ubebaji mizigo kwa kiwango cha juu.
‘‘Ukienda mkoani ukienda vijijini kuna watu wanawatumikisha watoto lakini huenda tukawapatia adhabu ambazo kwa namna moja ama nyingine pengine wao wenyewe hawana uelewa nazo kwahiyo nafikiri pia semina elekezi kupitia wizara husika ziweze kufanyika na majarida mbalimbali yanayoendelea kuwaelekeza watu juu ya haki za watoto na vitu gani watoto wanatakiwa wafanyiwe,’’ amesema mwanasheria Vicent Saguda kutoka Dar es Salaam
Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika kwa mwaka 2023 yamebebwa na kauli mbiu isemayo “Zingatia Usalama wa Mtoto katika Ulimwengu wa Kidijitali”. ikielekeza kuweka mazingira salama na kuchukua tahadhari dhidi ya watoto wakati wanapokuwa mitandaoni.
Imetayarishwa na Amri Ramadhani, VOA , Dar es Salaam.
Forum