Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Septemba 13, 2024 Local time: 20:20

Kenya, Tanzania, Rwanda na Uganda zapendekeza uwekezaji mkubwa katika kilimo na miundo mbinu.


Waziri wa fedha wa Kenya Njuguna Ndung'u awasilisha bajeti ya serikali bungeni
Waziri wa fedha wa Kenya Njuguna Ndung'u awasilisha bajeti ya serikali bungeni

Mawaziri wa fedha wa nchi za Afrika Mashariki wamewasilisha bajeti za serikali zao wakipendekeza uwekezaji mkubwa katika sekta za maendeleo, na wakati huo huo kuongeza kodi katika baadhi ya sekta.

Licha ya wabunge wa upinzani, Alhamisi, kuondoka bungeni kususia usomaji wa makadirio ya Bajeti ya mwaka wa Fedha wa 2023/24, Waziri wa Fedha Njuguna Ndungu aliwasilisha bajeti hiyo ya shilingi trilioni 3.67 ambayo ni ya kwanza katika utawala wa rais William Ruto, licha ya hali ngumu ya kiuchumi hii ni bajeti kubwa zaidi kuliko zote katika historia ya Kenya.

Waziri w Kenya Njuguna Ndung'u awasilisha bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2023/24 mjini Nairobi
Waziri w Kenya Njuguna Ndung'u awasilisha bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2023/24 mjini Nairobi

Bajeti inalenga kupunguza gharama za maisha, kuongeza ajira, ustawi wa jamii, kupanua wigo wa kodi kuzalisha mapato zaidi na kufikia mgawanyo ulio sawa wa mapato kwa raia wa Kenya, alieleza Waziri wa Fedha Njuguna Ndun’gu mbele ya bunge la taifa.

Aidha, Waziri huyo ameeleza kuwa bajeti hiyo pia inalenga kuimarisha kilimo, biashara ndogo ndogo na za kati, kuwezesha upatikanaji wa nyumba na makazi bora, na serikali kuwekeza katika huduma za afya na kiwango chake cha matumizi ya kawaida ni shilingi trilioni 2.53 huku shilingi bilioni 743 zikiwa zimetengwa kwa ajili ya maendeleo.

Bejeti hii inalenga kufikia mapato ya shilingi trilioni 2.9 ambayo ni asilimia 18.2% ya pato la taifa, inatajwa kuwa na azma ya kuwezesha ukuaji wa nguzo kuu ikiwa ni pamoja na miundombinu, viwanda, uchumi wa samawati, sekta ya huduma, mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa, elimu na mafunzo, ajenda ya wanawake, ajenda ya uwezeshaji na maendeleo ya vijana, ulinzi wa kijamii, michezo, utamaduni na sanaa.

Serikali ya rais Ruto, katika bajeti hiyo ya shilingi bilioni 300 zaidi ya mwaka wa 2023/24, inalenga kuongeza juhudi za kukusanya mapato kwa lengo la kufikia shilingi trilioni 4. Ili kufanikisha hili, inataraji kutekeleza mseto wa hatua za kodi na mageuzi ya sera ya ukusanyaji wa mapato.

Ripoti hii imetayarishwa na Kennedy Wandera, VOA Nairobi.

Tanzania kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo

Serikali ya Tanzania imepanga kutumia shilingi trilioni 44.39 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 katika miradi ya maendeleo na matumizi ya kawaida katika bajeti iliyosomwa Alhamisi Bungeni na Waziri wa fedha na Mipango Dkt Mwigulu Nchemba.

Mwigilu Nchemba, waziri wa fedha wa Tanzania asoma bungeni bajeti ya mwaka wa fedha wa 2023-2024
Mwigilu Nchemba, waziri wa fedha wa Tanzania asoma bungeni bajeti ya mwaka wa fedha wa 2023-2024

Akiwasilisha bajeti hiyo ya mwaka wa fedha 2023/2024, mjini Dodoma waziri wa fedha na mipango Mwigulu Nchemba ameiita ni ya kimkakati yenye lengo la kuwafikia wananchi wa kipato cha chini kwa kuongeza bajeti zaidi katika sekta muhimu ikiwemo kilimo hususan sekta ya umwagiliaji, usalama wa chakula, mifugo na uvuvi, miundombinu, afya pamoja na nishati ya umeme hususan vijijini.

Waziri huyo wa fedha amependekeza marekebisho kadhaa ya kodi katika kuongeza pato la serikali na pia kutoa unafuu katika sekta mbalimbali kwa lengo la kuchochea shughuli za kiuchumi na biashara.

Hata hivyo Dtk. Nchemba amesema licha ya changamoto mbalimbali bado kuna mwamko mdogo katika ulipaji kodi huku akionya mamlaka husika za ukusanyaji kodi kuacha kufunga biashara za wateja wakati wa migogoro ya kikodi.

Akizungumzia mfumuko wa bei Dkt Nchemba amesema umeendelea kuwa ndani ya lengo la wigo wa kuwa chini ya asilimia tano.

Amesema Mwaka 2022, mfumuko wa bei ulifikia wastani wa asilimia 4.3 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.7 mwaka 2021. Aidha, mfumuko wa bei hadi mwezi Mei, 2023 umebaki kama ilivyokuwa katika kipindi hicho hicho mwaka 2022 ikiwa ni wastani wa asilimia 4.0.

Ripoti imetayarishwa na Dina Chahali VOA, Dar es Salam.

Forum

XS
SM
MD
LG