Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Septemba 21, 2024 Local time: 07:09

Mgomo wa Soko la Kariakoo: Kamati kuwakilisha kero za wafanyabiashara


Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa alipolitembelea soko la Kariakoo lililopo katika jiji la Dar es Salaam. Picha na Global Publishers TV.
Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa alipolitembelea soko la Kariakoo lililopo katika jiji la Dar es Salaam. Picha na Global Publishers TV.

Kamati iliyoundwa na waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa kufuatia mgomo wa wafanyabiashara katika soko maarufu la Kariakoo inatarajia kuwasilisha maoni ya kero za wafanyabiashara Alhamisi.

Mjumbe aliye karibu na kamati hiyo ameiambia Sauti ya Amerika, kwamba kamati hiyo imekamilisha majukumu yake ya kukusanya maoni na kero za wafanyabiashara kutoka mikoa mbali mbali, pamoja na taasisi husika zinazolalamikiwa ikiwemo mamlaka ya Bandari na na ile ya kodi (TRA).

Kamati “iko tayari kuwakilisha ripoti muda wowote itakapopewa ruhusa ya kukutana na waziri mkuu” alisema mjumbe huyo ambae hakutaka kutajwa.

Kamati hiyo yenye jumla ya wajumbe 14 kutoka chama cha wafanyabiashara, na mamlaka husika za serikali, ilipewa mpaka kesho, tarehe 8 mwezi June kukamilisha ripoti yake baada ya kupokea malalamiko na matakwa ya wafanyabiashara kufuatia mgomo wa siku tatu katika soko la Kariakoo lenye mchango mkubwa katika uchumi wa jiji la Dar es Salaam.

Miongoni mwa malalamiko ya wafanyabiashara ni mrundikano wa kodi zinazotozwa na mamlaka ya mapato TRA pamoja na rushwa iliyokithiri na ukosefu wa muongozo unaoeleweka wa malipo ya kodi kwa bidhaa zinazoingizwa kutoka nchi za nje.

Ukosefu wa kiwango maalum cha ushuru wakati wa utoaji wa bidhaa kutoka bandarini husababisha rushwa kutokana na mfumo holela wa utozaji kodi wa njia ya majadiliano, wanadai wafanyabiashara.

Alipokutana na wafanyabiashara wa soko hilo mwezi uliopita Waziri Mkuu ameahidi kuendelea kutatua changamoto zinazowakera wafanyabiashara nchini. Na ameiagiza TRA kusitisha kazi za kikosi kazi chake "Task Force" ambacho kilikuwa kinaendesha zoezi la kuwakamata wafanyabiashara katika soko la Kariakoo bila ya kufuata kanuni au sheria.

MARIAM MNIGA, SAUTI YA AMERIKA, WASHINGTON DC.

Forum

XS
SM
MD
LG