Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Julai 14, 2024 Local time: 08:18

Tanzania haijatoa kipaumbele kwa maji


Mwanaume akiuza chupa za maji ya kunywa katika jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania, tarehe 23 Oktoba , 2015. PICHA N AFP / DANIEL HAYDUK.
Mwanaume akiuza chupa za maji ya kunywa katika jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania, tarehe 23 Oktoba , 2015. PICHA N AFP / DANIEL HAYDUK.

Upatikanaji wa huduma za maji safi na salama unaendelea kuwa changamoto na kikwazo kwa maendeleo ya wananchi wanaoishi pembezoni mwa miji ikidaiwa serikali kutotilia mkazo suala la upatikanaji wa maji katika maeneo hayo.

Tatizo la maji ni changamoto inayo wakabili wananchi kwa miaka mingi hususan wanawake wanaoishi vijijini ambao hulazimika kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo, wakati ukame umekuwa ukitajwa kuchangia ongezeko kwa tatizo hilo.

Serikali ya Tanzania inafanya utaratibu wa kutekeleza malengo yake ya upatikanaji wa maji safi vijijini kwa asilimia 85 na kwa maeneo ya mijini kwa asilimia 95 ifikapo mwaka 2025.

Mamlaka za maji mijini na vijijini zinakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazo changia ukosefu wa maji katika kaya, suala ambalo wananchi wanadai serikali haijalipa kipaumbele. Hivyo kusababisha wanawake kutembea umbali mrefu kutafuta maji.

Mbali na rasilimali nyingi za maji zilizopo nchini, Tanzania bado inashindwa kutatua tatizo la maji kwa wananchi wake ambao baadhi hupata maji kwa mgao, huku wengine wakitegemea vyanzo asili visivyo salama hususan maeneo ya vijijini.

Akizungumza na Sauti ya Amerika, Sophia Onesmo mkazi wa kijiji chaTanganyika mkoani Tanga amesema matumizi yake ya maji na bili anayoletewa hailingani, na kuongeza kuwa bili ya maji ya kila mwezi iko juu pamoja na kwamba maji hukatika mara kwa mara na kurudi usiku wakiwa wamelala.

“Unakuta mwezi mzima umetumia maji angalau galoni ishirini au hata kumi hazifiki lakini unajikuta bili unayoletewa ni ya shilingi elfu kumi na tano au elfu ishirini” alisema Sophia.

Changamoto hii ya maji inayowakabili wananchi inaonekana kuchangiwa na baadhi ya viongozi wa juu wenye dhamana katika mamlaka za maji kutokuwa waadilifu wakati baadhi yao kulichukulia suala hili kuwa la kawaida.

Aidha Wizara ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira imeombwa kutopokea ripoti za wakurugenzi wa mamlaka hizo, badala yake ipokee maoni kutoka kwa wafanyakazi wa chini.

Juma Msimbe mmoja ya wafanyakazi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira jijini Tanga aliiambia Sauti ya Amerika kuwa “Waziri wa Maji Jumaa Aweso asiishie kupokea ripoti za miradi mbalimbali za maji nchini, vilevile pia awe na utaratibu wa kuonana na watumishi ngazi za chini ili kuweza kupata maoni yao ili kuongeza ari na nguvu ya utendaji zaidi ili kuboresha huduma ya maji nchini”.

Kulingana na Wizara ya maji, kiwango cha upatikanaji wa maji kimeongezeka kutoka asilimia 70.1 hadi 77 kwa vijijini na kati ya asilimia 84 hadi 88 kwa mijini, lakini bado wananchi wanaitaka serikali kutekeleza ahadi zake kuhusiana na tatizo la maji ili kuondokana na kero hiyo.

XS
SM
MD
LG