Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Desemba 06, 2024 Local time: 10:13

Tanzania, Burundi na Uganda zinautaka Umoja wa Mataifa kuunga mkono juhudi za kuleta amani DRC


Wanajeshi na polisi wa jamhuri ya kidemokrasia ya Congo wakiwa Rutshuru, siku chache baada ya waasi wa M23 kupigana na wanajeshi wa serikali. April 3, 2022 PICHA: AFP
Wanajeshi na polisi wa jamhuri ya kidemokrasia ya Congo wakiwa Rutshuru, siku chache baada ya waasi wa M23 kupigana na wanajeshi wa serikali. April 3, 2022 PICHA: AFP

Serikali ya Tanzania imesema kwamba ipo tayari kutuma wanajeshi wake popote pale duniani kwa ajili ya kulinda amani chini ya mpangilio wa Umoja wa Mataifa.

Haya ni kulingana na makamu wa rais wa nchi hiyo Dkt. Philip Mpango ambaye ameueleza Umoja wa Mataifa kwamba matatizo yanayoikumba dunia kwa sasa yanatokana na tamaa na ubinafsi.

Dkt. Mpango amesema kwamba Tanzania imekuwa ikichangia katika juhudi za kuleta amani kupitia njia za kidiplomasia na kijeshi, katika nchi mbalimbali chini ya kanuni za kimataifa.

Zaidi ya wanajeshi 2600 wa Tanzania wanashiriki katika juhudi za kuleta amani chini ya Umoja wa Mataifa katika mataifa mbali mbali ambako Umoja wa Mataifa una vikosi vyake, ikiwemo Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

“Jukumu la kulinda amani ni muhimu sana kwa ajili ya amani na usalama kote duniani. Tanzania inajivunia kuchangia wanajeshi wake katika nchi 5 kati ya 16 chini ya mpango wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kote duniani. Tanzania ipo tayari kuchangia wanajeshi wake inapoombwa kufanya hivyo. Tunashiriki kikamilifu katika maswala ya amani kama wanachama wa baraza la usalama la Umoja wa Afrika, Jumuiyaya Afrika Mashariki na SADC” amesema mpango

Burundi pia ipo tayari kuendelea kutuma wanajeshi nchi nyingine

Kauli ya Tanzania iimefanana na ile ya Burundi, ambapo rais wa nchi hiyo Evariste Ndayishimiye, naye ameahidi kwamba nchi yake itaisaidia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kupambana na makundi ya waasi mashariki mwa nchi hiyo.

Ndayishimiye, ambaye wanajeshi wake tayari waliingia Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kupambana na waasi wa Red Tabara, na kuchangia katika kikosi cha jeshi la Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuleta amani Mashariki mwa DRC, ameiomba jumuiya ya kimataida kuisaidia DRC.

“Burundi haitachoka kuchangia wanajeshi wake wa ajili ya amani katika nchi zenye vita. Tutafanya hivyo kwa kuzingatia kanuni za Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na mikataba mingine. Kwa sasa wanajeshi wetu wanalinda amani nchini Somalia na Afrika ya Kati. Burundi imejitolea kusaidia kurejesha amani huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo chini ya makubaliano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nachukua fursa hii kuomba jumuiya ya kimataifa kuunga mkono mkono makubaliano ya Nairobi, kuisaidia DRC.”

Uganda inataka Afrika iwe na uwakilishi katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Lakini Makamu wa rais wa Uganda Jessica Alupo, amesisitiza kwamba mafanikio ya kiusalama na maendeleo ya jumla yanastahili kumshirikisha kila mtu, akisisitiza kwamba Afrika inahitaji kuwakilishwa katika maamuzi ya juu ya Umoja wa Mataifa.

Uganda ina jumla ya wakimbizi milioni 1.5 wengi wao kutoka nchi Jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Wamekimbia vita vya zaidi ya miaka 20 ambavyo vinatekelezwa na zaidi ya makundi 100 yaliyo mashariki mwa nchi hiyo.

“Kuna haja ya kufanyika mabadiliko katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa haraka. Hali halisi ya kisiasa inahitaji mabadiliko makubwa sana katika baraza la usalama ili kuwepo uwakilishi ulio sawa. Afrika yenye watu billion 1 na zaidi ya asilimia 70 ya maswala yanayojadiliwa kwenye baraza hilo yanatoka Afrika, haina mwakilishi wa kudumu. Isitoshe, wawakilishi katika nafasi zisizo za kudumu ni wachache.” Amesema makamu wa rais wa Uganda Jessica Alupo.

Juhudi za amani Sudan kusini

Sudan Kusini, ambayo pia iameahidi wanajeshi 750 kwa ajili ya kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, imesema kwamba kuna matumaini makubwa kwamba hali ya utulivu itaendelea kuwepo nchini humo, baada ya miaka ya malumbano ya kisiasa na vita.

Makamu wa rais Hussein Akol amesema kwamba pande zilizokuwa zikihasimiana zimekubali kutekeleza mkataba wa amani wa mwaka 2018 na kuhakikisha kwamba nchi hiyo ina amani, na kuzisaidia nchi Jirani zinazokumbwa na misukosuko.

XS
SM
MD
LG