Kwa mujibu wa msemaji wa Symbion Julie Foster, Symbion imefungua kesi kwa ajili ya kutafuta usuluhisho mahakamani Jumatatu, limeripoti gazeti la Daily Nation, Kenya.
Amesema kwa zaidi ya mwaka mmoja juhudi za kutafuta ufumbuzi juu wa utata unaohusu uhalali wa mkataba wa manunuzi ya umeme wa miaka 15, kwa njia ya urafiki zimeshindikana, “Hatuna njia nyingine.”
“Mwezi mmoja uliopita, tuliwaandikia Tanesco kuwapa notisi kwamba hatutakuwa na njia mbadala zaidi ya kusitisha mkataba. Notisi hiyo imeisha muda wake March 3, lakini Tanesco hawajajibu chochote. Wameendelea kupuuzia madai ya Symbion.
“Tulivuta subira kwa wiki moja zaidi na bado hatukupata jawabu lolote na hivyo hatimaye bila ya kupenda tuliamua kwenda mahakama ya kimataifa Machi 13. Mkataba wa ununuzi wa umeme umefutwa na kiwango kinacho daiwa ni dola 561 milioni,” amesema Foster katika tamko lililo tumwa kwa gazeti la The Citizen.
Mkataba huo wa PPA wenye utata ulisainiwa Disemba 2015, ukiwapa Symbion mkataba wa muda mrefu kuwazalishia umeme Tanesco wenye MW 112 kupitia mitambo ya kuzalisha umeme inayoendeshwa kwa gesi kwa kipindi hadi Disemba 2030.
Hata hivyo, mnamo Januari 26, 2016 Tanesco iliwaandikia Symbion, ikisema kuwa mkataba wa PPA umesimamishwa. Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco wa zamani Felchesmi Mramba alieleza hapo awali mwaka jana kuwa serikali ilielekeza “isimamishe” mahusiano ya kibiashara na Symbion na baadae akasema hakuwa tayari kuzungumzia tatizo hili kwenye vyombo vya habari.
“Hatuwezi kuacha mtambo wa umeme mkubwa kama huu wenye kuzalisha MW 120 ukasimama wakati Tanzania inauhaba wa umeme. Symbion walikuwa wakiendesha mtambo huo kwa miaka sita na siku zote ilikuwa ikiidai Tanesco kiwango kikubwa cha fedha. Kituo hicho cha Symbion kilikuwa kinaiuzia umeme Tanesco kwa gharama nafuu mno, kwa hivyo ni aibu kuona kwamba Tanesco imetusukuma nje ya biashara bila sababu za msingi, amesema Foster.
“Kwa upande wetu Symbion huu ni wakati mbaya sana na hatujaridhishwa na hili kabisa. Kama kila mmoja wetu anavyojua sisi tumekuwa mstari wa mbele kuisaidia Tanzania na pamoja na mgogoro kati yetu na Tanesco, siku zote tutaitakia Tanzania na Serikali yake mazuri.”
Katika hii hatua iliochukuliwa na Symbion kufikisha tatizo hili mahakama ya kimataifa, Septemba mwaka jana, Kituo cha Kimataifa katika kusuluhisha matatizo ya uwekezaji (ICSID) iliitaka Tanesco kulipa dola milioni 148.8 kwenye benki ya Standard Chartered –Hong Kong kutokana na mgogoro unaohusiana na umiliki wenye utata wa kampuni ya IPTL.
Matatizo ya Tanesco yalianza baada ya serikali, Septemba 2013, katika hali ya utata ilipolipa zaidi ya shilingi bilioni 440 (dola milioni 200) kwa kampuni ya Pan African Power Solutions Tanzania Limited (PAP) inayomilikiwa na Harbinder Sethi baada ya kutangaza kuwa ameinunua IPTL.
Fedha hizo zilitolewa kutoka katika akaunti ya escrow huko eneo la Tegeta ambapo akaunti hiyo ilikuwa imefunguliwa na Benki Kuu ya Tanzania baada ya Tanesco kufungua mashtaka katika ICSID ikidai inalipishwa kiwango cha juu na kampuni ya IPTL. Pande zote zilikubaliana kuwa malipo yapelekwe kwenye akaunti hiyo mpaka pale ufumbuzi utapopatikana.