Kituo cha televisheni cha Al Arabiya kimeonyesha picha za moshi mzito ukitoka kwenye jengo moja katika mji mkuu kutokana na mfululizo wa milipuko ya mabomu yenye sauti kubwa.
Kuzuka ghafla kwa mapigano mwishoni mwa wiki baina ya majenerali wawili wa juu wote wanaungwa mkono na maelfu ya wapiganaji wenye silaha nzito, hali hiyo imewasababisha watu kukwama katika nyumba zao au mahali popote wanapoweza kupata hifadhi.
Bidhaa muhimu zimeanza kupungua na hospitali kadhaa zimelazimika kufungwa. Wakati huo huo msemaji wa vikosi vya Sudan alisema Jumanne jeshi lilikuwa limeshika udhibiti wa shirika la utangazi la serikali.
Televisheni ya Sudan inayoendeshwa na serikali ilirusha mazungumzo ya simu na Brigedia Jenerali Nabil Abdullah ambapo alidai hali ilikuwa imedhibitiwa kabisa.
Aliongeza kusema kuwa jeshi la Sudan halitaki kupanua operesheni zake katika hatua iliyopo sasa. Jeshi na kikosi cha RSF walikuwa wanapigana pia katika miji mikubwa katikati kuzunguuka nchi hiyo ikiwemo magharibi mwa Darfur na sehemu ya kaskazini na mashariki zinazopakana na Misri na Ethiopia.
Mapigano ni sehemu ya kugombea madaraka kati ya Jenerali Abdel Fattah Burhan mkuu wa vikosi vya jeshi, na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo mkuu wa RSF.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema Jumanne kwamba mwanadiplomasia wa juu wa Marekani alishambuliwa huko Sudan na amesisitiza umuhimu wa kusitisha mapigano.
Blinken alizungumza katika mji wa kifahari wa Karuizawa huko Japan muda mfupi baada ya kufunga mazungumzo ya kundi la G7.