Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Mei 29, 2024 Local time: 11:40

Chadema wasusia baada ya mwenzao kutolewa Bungeni


John Mnyika
John Mnyika

Wabunge wa Chadema walitoka nje baada ya mwenzao Mbunge wa Kibamba John Mnyika kutolewa nje ya Bunge nchini Tanzania Ijumaa kwa mabavu na askari.

Wakati askari hao wakijaribu kumnasihi Mnyika kutoka nje ya ukumbi wa Bunge kwa hiari yake, spika Job Ndugai alisema: “Nyinyi askari gani toa nje, askari wa wapi hawa, nyinyi ni askari au raia, ukiambiwa toa mtu toa mtu…,” alisema kwa hasira.

Baada ya karipio hilo la spika askari hao waliongeza kasi na kumburuza Mnyika hadi nje huku Mbunge wa Kawe Halima Mdee akijaribu kuwafikia askari na kuzuia Mnyika asitolewe nje.

Wakati huo huo Mbunge wa Bunda Mjini Esther Bulaya alianza kuhamasisha wabunge wote wa upinzani watoke nje ya ukumbi, jambo ambalo pia lilimuudhi Spika.

Mnyika amefungiwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa muda wa wiki moja kwa madai ya kuwa alikaidi amri ya kiti cha spika kinyume na Kanuni za Bunge.

Pamoja na mbunge huyo, pia wabunge wa Chadema Mdee na Bulaya, hatma yao itajulikana Jumatatu ijayo, baada ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuwajadili.

Sakata hilo, liliibuka wakati mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM) akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/18.

Mnyika aliomba utaratibu kwa Spika, na kumueleza Lusinde kuwa hoja ya upinzani si kupinga hatua hiyo ya kuchunguza makinikia.

Aliitaka serikali isijikite katika eneo hilo dogo la mchanga na badala yake iweke nguvu zaidi kwenye wizi mkubwa wa madini ya dhahabu yenyewe unaofanyika migodini.

Hata hivyo, Ndugai alimweleza Mnyika kuwa hakuitumia vyema kanuni ya kuomba utaratibu, kwani alitakiwa ataje kanuni iliyovunjwa na mchangiaji (Lusinde) kisha akiachie kiti kiamue na si kutoa taarifa kama alivyofanya.

Wakati Mnyika anakaa ili kumpisha Lusinde aendelee kuchangia, sauti ya mmoja wa wabunge aliyewasha kipaza sauti ilimwita Mnyika mwizi, jambo lililomfanya mbunge huyo kuwasha kipaza sauti chake wakati mwenzake akiendelea kuchangia, akitaka mwenye kutoa kauli hiyo athibitishe mbele ya Bunge hilo.

Mnyika hakukubali na aliendelea kupaza sauti yake na kutaka aliyemwita mwizi achukuliwe hatua, wakati huo wote spika Ndugai alikuwa akimuonya kwa zaidi ya mara tatu, ndipo aliapoamuru askari wamtoe nje.

“Mheshimiwa Mnyika kwa mara ya mwisho nakutaka ukai chini. Uliomba utoe kuhusu utaratibu kwa mheshimiwa Lusinde, nimekupa nafasi hiyo. Habari ya mimi kuwa na masikio mia kusikiliza kila mtu anaongea nini bungeni hilo haliwezekani,” alisema Spika

Spika aliendelea kumuonya Mnyika kwa kumwambia: “Don’t dare me”, akitafsiri kuwa usinijaribu, wakati kulikuwapo na sauti zilizokuwa zikisema kuwa mtoe nje.

Hapo ndipo spika alisema: “Sergeant at arms leo ni siku gani, Ijumaa, huyu wiki nzima nisimuone hapa, aliamrisha spika.

XS
SM
MD
LG